
Na WMJJWM - Windhoek, Namibia
Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizo na Mwongozo wa Kitaifa wa Uratibu wa Wajane, uliyozinduliwa Juni 23, 2025, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wajane Afrika huko Zanzibar. Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, alipohudhuria mkutano huo jijini Windhoek, Namibia, Septemba 3, 2025, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Gwajima amesema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya 2022, wajane nchini wanakadiriwa kufikia milioni 1.3 sawa na asilimia 4.4 ya wanawake wote, na kwamba Mwongozo wa Kitaifa unaainisha namna ya kukabiliana na mila na desturi zinazowanyima haki za urithi, ardhi, mali, elimu na ushiriki kwenye maendeleo ya jamii.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka mikakati thabiti ikiwemo Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake, mikopo isiyo na riba kwa wajane, huduma za kisheria bure, na maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani kila Juni 23 kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki zao.
Katika hotuba ya ufunguzi, Naibu Waziri wa Usawa wa Kijinsia na Ustawi, Mheshimiwa Linda Mbale, alisema ujane mara nyingi huchukuliwa kama adhabu ya kijamii badala ya msiba, jambo linalosababisha unyanyapaa, hivyo kuna haja ya sera na mikakati mahsusi ya kuwasaidia wajane.
Mkutano huo uliandaliwa na Umoja wa Wajane wa Afrika ukiwa na kaulimbiu “Widowhood in Africa: Building a Sustainable Culture” na kujadili masuala muhimu kama haki za wajane, ushiriki wao kwenye uchumi na siasa, elimu, afya, makazi, na uundaji wa sera na sheria zinazowalinda. Katika mkutano huo, Mama Anna Mkapa mjane wa aliyekua Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa alipata heshima ya kuzindua Mpango wa Afrika wa Ukuaji na Maendeleo ya Wajane.
Vilevile, Umoja wa Mataifa kupitia Mwakilishi wake nchini Namibia, Mhe. Hopolang Phororo, umeahidi kuendelea kushirikiana na nchi wanachama kulinda haki za wajane. Mwenyekiti wa Umoja wa Wajane wa Afrika, Dkt. Hope Nwakwesi, alisifu jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumshukuru Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Wajane Afrika.






No comments:
Post a Comment