TAWA YAMNASA SIMBA MLA MIFUGO KONDOA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 7, 2025

TAWA YAMNASA SIMBA MLA MIFUGO KONDOA.



Na Mwandishi wetu, Dodoma


Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imefanikiwa kumkamata simba jike akiwa hai baada ya mfululizo wa mashambulizi ya wanyama hao kuua zaidi ya mifugo 20 katika Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma.

Simba huyo aliingia kwenye rada za askari wa TAWA majira ya saa 4 usiku, Septemba 6, 2025, katika kijiji cha Chemchem, kufuatia msako mkali uliodumu kwa siku tatu ambapo mnyama huyo alijikuta tayari amenasa katika mtego maalum uliowekwa na Askari hao.

Imeripotiwa kuwa wanyama simba wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mifugo katika vijiji vya Chemchem na Iyoli, Kata ya Kingale ambapo katika nyakati tofauti waliua ng’ombe wawili na punda mmoja na baadae kuua ng’ombe 18 katika gereza la king'ang'a. Aidha, waliripotiwa pia kuua mbuzi wawili katika kijiji cha Iyoli.

Kutokana na ongezeko la matukio hayo, Mamlaka ilianza operesheni ya kudhibiti simba hao kwa kutumia Askari wake na baadaye kuongeza timu ya madaktari wa wanyama. Hatimaye, mnamo septemba 6 majira ya saa 4 usiku, simba jike alikamatwa kwa kutumia mbinu za kitaalamu.

Afisa Mhifadhi Daraja la Kwanza ambaye pia ni daktari wa wanyamapori Masalu Makoye Mroje, alisema simba huyo atasafirishwa kwenda eneo la mbali lenye mazingira rafiki, ili kuzuia madhara kwa wananchi na mifugo yao.

Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Chemchemi, Kata ya Kingale, wilayani humo, wameipongeza Serikali kupitia TAWA kwa uwajibikaji wake katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori waharibifu, hususan kitendo cha kumdhibiti simba huyo aliyezua taharuki kwa wananchi.

"Tumekuwa na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu Kwa muda sasa, Simba walikula mifugo yetu na kutusumbua lakini leo amani imerejea baada ya TAWA kufanikiwa kumdhibiti mnyama huyu na kutuahidi kufuatilia Simba wengine ili kuwaondoa kijijini kwetu" alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemchem Bw. Mashaka Said Funga

Aidha TAWA inaendeleza uchunguzi na ufuatiliaji ili kubaini kama kuna simba wengine katika maeneo hayo ili waweze kuondolewa, na kuwaomba wananchi kutoa taarifa haraka iwapo watawaona.



No comments:

Post a Comment