
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema jamii sasa inatambua nafasi muhimu ya Wakadiriaji Majenzi katika kusimamia miradi ya ujenzi, kujenga ushirikiano mzuri na Serikali, pamoja na kuongeza thamani na ubora wa miradi ya kitaifa na binafsi.
Dkt. Msonde ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa 31 wa Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi (TIQS) ambapo ameipongeza taasisi hiyo kwa kazi kubwa ya kutoa mafunzo na kuongeza ujuzi kwa wanachama wake ili kuendelea kuchochea ukuaji wa taaluma na maendeleo ya Taifa.
Aidha, Dkt. Msonde amesema Wizara ya Ujenzi ina jukumu kubwa la kupitia Sera na kuendeleza ubunifu katika Sekta ya Ujenzi, huku akibainisha kuwa kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu imekuja kwa wakati muafaka.
Pia ameeleza kuwa mabadiliko ya Sheria za AQRB yamelenga kutambua rasmi fani ya Ukadiriaji Majenzi na kuifanya sehemu ya ajira katika sekta hiyo.
“Uwepo wenu umechochea mafanikio makubwa katika usimamizi wa miradi na ubora wa mikataba ya ujenzi, jambo lililosaidia miradi kukamilika kwa wakati na kwa gharama halisi,” alisema Dkt. Msonde.
Aliongeza kuwa Wakadiriaji Majenzi wanapaswa kushiriki kikamilifu si tu katika miradi ya serikali, bali pia katika miradi ya taasisi na binafsi, ili kuhakikisha fedha zinatumika kulingana na thamani ya miradi husika. Pia aliwahimiza kujadili na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha sera na sheria za sekta ya ujenzi
Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi, QS Bernad Ndakidemi, alisema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1987 na hadi sasa ina wanachama 1,174, huku jitihada zikiendelea za kuwashawishi wataalamu walioko mitaani kujiunga.
QS Ndakidemi alisisitiza kuwa Wakadiriaji Majenzi wana nafasi muhimu katika kuhakikisha majengo yanakamilika kwa wakati na kwa gharama halisi. Alitoa rai kwa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha taasisi zote zinazohusika na ujenzi zinawatumia wataalamu hao ili kuongeza ubora na thamani ya miradi, pamoja na kuondoa mkanganyiko wa kitaaluma kati ya wahandisi na wakadiriaji majenzi.
“Kuna changamoto ya miradi kutowahusisha Wakadiriaji Majenzi kwa kudhani kuwa wahandisi pekee wanatosha. Hali hii imekuwa ikisababisha miradi kusuasua na kutokamilika kwa wakati. Ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha, ni lazima kila mradi uhusishe Mkadiriaji Majenzi,” alisema QS Ndakidemi.
Naye, Kaimu Msajili wa AQRB Arch. Dkt. Daniel Gittu Matondo, amesema mkutano huo wa 31 umelenga kubadilishana mawazo na kuweka mikakati thabiti ya usimamizi wa miradi kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Amesema Bodi ya AQRB itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi ili kuhakikisha taaluma ya Ukadiriaji Majenzi inaleta manufaa makubwa kwa taifa.









No comments:
Post a Comment