
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Pangani Mkoani Tanga na Waziri wa Maji wa serikali ya awamu ya sita Mhe. Jumaa Aweso amesema katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa serikali ya awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Trilioni 3 kwa wizara ya Maji ili kujenga miradi ya Maji nchini, trilioni moja ikitumika kwenye miradi ya maji Dar Es Salaam.
Aweso ametoa takwimu hizo leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 wakati wa Mkutano wa Kampeni za Mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Viwanja vya Tanesco Buza, Wilayani Temeke, akisema uwekezaji huo mkubwa umewezesha pia kumaliza changamoto ya maji kwenye maeneo ya Buza, Temeke, Mbagala na Chamanzi.
Aweso pia amesema uwekezaji huo ndani ya miaka minne ya Dkt. Samia umesaidia pia kuongeza mtandao wa maji katika Mkoa huo wa Dar Es Salaam kutoka Kilomita 3,000 alizozikuta hadi kufikia Kilomita 7,000, sawa na ongezeko la Mtandao wa Maji wa Kilomita 4,000 kwa miaka minne.
Ameeleza kuwa ndani ya miaka minne serikali ya Dkt. Samia pia imewekeza zaidi ya Bilioni 400 kwaajili ya mifumo ya majitaka kwenye Mkoa wa Dar Es Salaam.
Waziri Aweso pia amezungumzia ugumu uliokuwepo wa utekelezaji wa mradi visima vya Mpera na Kimbiji Wilayani Kigamboni pamoja na utegemezi wa Mkoa wa Dar Es salaam kwenye vyanzo vya maji vya Ruvu chini na Juu, akisema miaka minne ya Dkt. Samia, wametekeleza pia mradi mkubwa wa maji wa shilingi Bilioni 21 uliotoa maji Kigamboni na kuhudumia wananchi wa Wilaya ya Temeke na katikati ya Jiji la Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment