BAJAJI NA BODABODA DODOMA WADHIHIRISHA WAKO TAYARI KUSHIRIKI UCHAGUZI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 18, 2025

BAJAJI NA BODABODA DODOMA WADHIHIRISHA WAKO TAYARI KUSHIRIKI UCHAGUZI.




Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kushiriki katika zoezi la kupiga kura, huku akiwaomba kumpigia kura yeye, Rais Samia Suluhu Hassan, na wagombea wote wa CCM katika ngazi ya udiwani.

Akizungumza leo Oktoba 13, 2025 jijini Dodoma wakati wa muendelezo wa kampeni zake katika kata ya Tambukareli, Mavunde aliwaasa maafisa usafirishaji (madereva bodaboda na bajaji) wa jimbo hilo kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura bila hofu au vizuizi vyovyote.

“Ndugu zangu maafisa usafirishaji, nendeni mkatimize haki yenu ya kimsingi ya kuchagua viongozi wenu. Hii ni haki ya kikatiba, na asije mtu akazuia haki yenu. Naomba mjitokeze kwa wingi Oktoba 29 mkapige kura,” amesema Mavunde.


Katika hotuba yake, Mavunde aliwaahidi maafisa usafirishaji kuwa akipewa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia, atashirikiana na viongozi wao akiwemo Mwenyekiti wa maafisa usafirishaji mkoa wa Dodoma ili kuboresha mazingira yao ya kazi na kuhakikisha jeshi la polisi na mgambo wa jiji wanapunguza usumbufu kwao.

Aidha, ameahidi kutekeleza miradi kadhaa ya kuboresha sekta ya usafirishaji ikiwemo Ujenzi wa mabanda mazuri katika vituo vyote vya bodaboda na bajaji ili wapate sehemu za kukaa na kujikinga na jua, Mpango wa umiliki wa pikipiki kuanzia mwezi Novemba 2025, madereva watasaidiwa kuondoka kwenye mfumo wa mikataba na kumiliki pikipiki zao kupitia utaratibu maalum wa mikopo, Kuendeleza programu ya “Tairi la Mama” itakayowawezesha madereva kununua tairi kwa bei nafuu ya kati ya shilingi 8,000 hadi 10,000, wakilipa kwa awamu na Kuwasaidia kupata viwanja vya kujenga makazi kwa mfumo wa malipo ya awamu.

“Mimi na nyinyi ni damu damu. Siwezi kuwaacha. Nitaendelea kuwa pamoja nanyi kushiriki matatizo na kero zenu,” alisema Mavunde huku akishangiliwa na mamia ya madereva waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.

Mavunde pia ameishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali maafisa usafirishaji, akibainisha kuwa tayari wamejengewa ofisi mpya eneo la Makole, jambo ambalo limewaweka mbele ukilinganisha na mikoa mingine.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa kata ya Tambukareli, Clinton Yona Mbazi, aliwahakikishia wananchi kuwa vijana wa kata hiyo wako tayari kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa Rais Samia, Mavunde, na wagombea wote wa CCM.

“Ifikapo Oktoba 29, sisi kama vijana tutaenda kupiga kura nyingi sana kwa mama yetu Dkt. Samia, na kwa mbunge wetu Anthony Mavunde. Tunatamani kata ya Tambukareli iwe ya kwanza kwa ushindi mkubwa ili tupate ofisi ya chama kama alivyoahidi,” alisema Mbazi.


Kampeni za CCM katika jimbo la Mtumba zimeendelea kwa kasi, huku Mavunde akipokelewa kwa hamasa kubwa katika kata mbalimbali anazotembelea, akiahidi kuendeleza maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo hilo.
















Naanan

No comments:

Post a Comment