
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema shilingi Bilioni 44. 9 za Kitanzania zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Kituo kikuu cha Mabasi Jijini Arusha pamoja na ujenzi wa masoko ya wafanyabiashara wadogo ya Morombo na Kilombero Jijini humo kama sehemu ya mpango wake wa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Dkt. Samia ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 02, 2025 wakati wa Mkutano wake wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu Jijini Arusha, akieleza kwamba katika kipindi chake cha miaka minne, serikali ya awamu ya sita pia ilifanikisha ujenzi wa soko la Mbauda, akieleza kwamba serikali pia inajenga soko jingine eneo la Bondeni City kwaajili ya wafanyabiashara wadogo, kwenye Mji unapojengwa Uwanja wa michezo na Kituo cha Mabasi.
Ameahidi pia kuendelea kutoa na kusimamia ipasavyo Mikopo ya asilimia kumi kutoka kwenye Halmashauri za Mkoa wa Arusha, akisema kufikia sasa jumla ya vikundi 853 vimenufaika na zaidi ya shilingi Bilioni kumi na milioni mia nne zimetumika kuwezesha Vikundi hivyo vya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Dkt. Samia kadhalika amesisitiza mpango wake wa kuanzisha mfuko maalumu ndani ya siku zake mia moja za awali madarakani ikiwa atachaguliwa, akisema mfuko huo utaanza na mtaji wa Bilioni 200 kwaajili ya kuwezesha biashara ndogo ndogo, fedha ambazo zitaendelea kuongezeka kulingana na hali ya uchukuaji mikopo na marejesho yake.



No comments:
Post a Comment