DKT. MPANGO: MAKUMBUSHO YA KISASA YA NGORONGORO KUKUZA UTALII WA KIHISTORIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 16, 2025

DKT. MPANGO: MAKUMBUSHO YA KISASA YA NGORONGORO KUKUZA UTALII WA KIHISTORIA


Na Mwandishi Wetu, Karatu


MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amezindua rasmi Makumbusho ya Urithi wa Kijiolojia ya Ngorongoro–Lengai, yaliyogharimu zaidi ya Sh. bilioni 35 ambayo yanatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa utalii wa kihistoria na kielimu nchini.

Makumbusho hayo yapo katika eneo la Ngorongoro–Lengai Geopark, linalotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama Geopark pekee Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili barani Afrika.

Akizungumza leo Oktoba 16,2025 katika uzinduzi huo wilayani Karatu, Dkt. Mpango amesema kukamilika kwa makumbusho hayo ni hatua muhimu katika kukuza utalii wa urithi na historia, sambamba na kutangaza vivutio vya asili vya Tanzania kimataifa.


“Geopark hii siyo tu hifadhi ya historia, bali ni chachu ya elimu, tafiti na maendeleo ya jamii zinazozunguka eneo hili,” amesema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha shughuli zote za utalii katika eneo hilo zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi na uendelevu wa mazingira, akisisitiza kuwa uharibifu wa mazingira unaweza kuathiri moja kwa moja ustawi wa sekta ya utalii.

Pia, ameagiza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kutoa mafunzo kwa watumishi watakaohudumu katika Geopark hiyo ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma kwa wageni.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema mradi huo ni wa kwanza wa aina yake barani Afrika chini ya mpango wa “Belt and Road Initiative”, na unadhihirisha ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Tanzania katika nyanja za utalii na utamaduni.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema eneo la Ngorongoro–Lengai limetambuliwa na UNESCO na pia limepata tuzo ya kivutio bora cha utalii Afrika kupitia World Travel Awards 2025 ni ishara ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Chana ameongeza kuwa mafanikio mengine makubwa ni pamoja na TANAPA na NCAA kupatiwa kibali cha kutumia hadi asilimia 51 ya mapato yao katika mwaka wa fedha 2025/26.

Kadhalika, amesema kuongezeka kwa watalii wa kimataifa kutoka 1,808,205 mwaka 2023 hadi 2,142,895 mwaka 2024, Watalii wa ndani wameongezeka kutoka 1,985,707 mwaka 2023 hadi kufikia 3,217,352 mwaka 2024.

No comments:

Post a Comment