
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ndani ya Miaka mitano ijayo ikiwa Chama chake kitapewa ridhaa ya kuunda serikali, watajenga daraja la Jangwani litakalokuwa na urefu wa Mita 390 pamoja na soko kubwa la kisasa katika eneo hilo kwaajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo.
Dkt. Samia amesema kufikia sasa tayati taratibu zote za kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo zimekamilika isipokuwa jambo moja pekee wanalolisubiri, akisema daraja hilo mbali ya kupendezesha Jiji la Dar Es Salaam, litarahisisha pia shughuli za usafiri na usafirishaji na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na Kijamii.
Dkt. Samia ametoa ahadi hizo leo Jumatano Oktoba 22, 2025 wakati wa Mkutano wa Kampeni za uchaguzi Mkuu wa Tanzania kwenye Viwanja vya Kecha, Kinyerezi, Wilayani Ilala Mkoani Dar Es Salaam, akiahidi pia ujenzi wa madaraja mengine Mkoani humo likiwemo daraja la Mzinga Wilayani Ilala.
Mgombea huyo pia amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025/30 imemuelekeza kujenga barabara za juu (Flyover) katika Makutano ya barabara Tabata, Buguruni na Fire ili kuondoa msongamano wa magari kwenye Jiji hilo lililo kitovu cha biashara Tanzania.
Katika hatua nyingine akizungumzia mafanikio yaliyopatikana Mkoani humo, Dkt. Samia amesema serikali yake pia imefanikiwa kujenga soko kubwa na la kisasa la Kariakoo mara baada ya jengo lililokuwepo awali kuungua moto, akisema kwasasa biashara zinafanyika vyema katika soko hilo kubwa linalotumika pia na wafanyabiashara na wanunuzi kutoka nje ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment