
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake ya awamu ya sita imeweka historia ya maendeleo makubwa wilayani Muleba, mkoani Kagera, kupitia miradi ya afya, elimu, miundombinu, kilimo, maji, nishati na biashara, ikionesha dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maisha bora.
Akihutubia malefu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Muleba Mjini kwenye Viwanja vya Zimbihile leo Jumatano Oktoba 15, 2025 Dkt. Samia amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM umeleta mabadiliko makubwa katika nyanja zote muhimu za kijamii na kiuchumi.
"Tuliahidi maendeleo yanayoonekana, na leo Muleba ni mfano wa kazi tulizozifanya. Tumeboresha hospitali, shule, barabara, umeme, na huduma za maji. Huu ni ushahidi kwamba Serikali ya CCM ni ya vitendo, si maneno,” amekaririwa akisema Dkt. Samia.
Katika sekta ya afya, Serikali ya awamu ya sita imekamilisha ujenzi wa majengo 22 katika Hospitali ya Wilaya ya Malahara, zahanati 16 katika vijiji vya Buhaya, Ilogelo, Kashasha, Buyaga, Kitua, Mulela, Kakoma, Burungura, Bihanga, Kabare, Kiholele, Buhuma, Kinagi, Kisana, Bulembo na Makongora, pamoja na vituo vya afya viwili katika kata za Kimwani na Ngenge.
Aidha, zimejengwa nyumba 20 za watumishi wa afya na kuimarishwa huduma za upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Kwa upande wa barabara, Dkt. Samia amesema Serikali yake imefanya matengenezo kwa kiwango cha lami katika barabara za Omundangara– Wapiwapi, Amanengo–Kijwire, Vijana–Bukono, Tukutuku–Kaigara na TANESCO–Afande, pamoja na matengenezo ya barabara za changarawe katika maeneo ya Kanyinya–Kaboya–Ntungamo, Mishambya–Rwamtukuza–Kabebya, na Bushonge. Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara mpya mijini na vijijini unaoendelea kukamilika.
Katika sekta ya elimu, Serikali imejenga na kukamilisha vyumba 321 vya madarasa ya shule za msingi, madarasa 300 ya sekondari, vyumba 47 vya maabara, mabweni 48, nyumba 41 za walimu, na matundu ya vyoo 1,198 katika shule mbalimbali wilayani Muleba. Vilevile, yamejengwa majengo sita ya utawala katika shule za msingi ili kuboresha mazingira ya ufundishaji.
Kwa upande wa kilimo, Dkt. Samia alibainisha kwamba Serikali imeendeleza shamba la vijana la kahawa lenye ekari 300, kuzalisha miche 20,000 ya kahawa, na kuongeza matumizi ya mashine bora za kilimo (matrekta kutoka 2 hadi 15) ili kuongeza uzalishaji. Aidha, imeanzishwa mpango wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia makusanyo ya halmashauri.
Sekta ya maji nayo imepata msukumo mkubwa kwa ujenzi wa miundombinu ya maji mjini Muleba, huku sekta ya mifugo ikinufaika kupitia kuboresha kitalu cha ufugaji wa kisasa, na utoaji wa huduma za chanjo kwa mifugo zaidi ya 470,000 wakiwemo ng’ombe, kuku na mbwa.
Kwa upande wa nishati, Dkt. Samia alieleza kuwa ujenzi wa kituo kidogo cha umeme (Switching Station) eneo la Ilemela unaendelea, ili kuboresha upatikanaji wa umeme Muleba nzima.
Pia, sekta ya biashara imeboreshwa kwa ujenzi wa majengo ya kisasa ya biashara (shopping mall) katika eneo la SIDO Muleba Mjini na ukamilishaji wa soko kuu la kisasa mjini humo.


No comments:
Post a Comment