Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Mkoani Singida kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema katika Miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali yake ya awamu ya sita imeweka rekodi ya kuajiri Vijana wengi zaidi na kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania wengi zaidi katika sekta mbalimbali kupita wakati mwingine wowote.
Mwigulu ametaja takwimu hizo leo Jumapili Oktoba 19, 2025 wakati wa Mkutano wa kampeni za Mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan, Sumbawanga Mjini kwenye Viwanja vya Kizwite Mkoani Rukwa, akimtaja Dkt. Samia kama kinara pia wa utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo na mwenye upendo mkubwa kwa watu wake.
Amemtaja Dkt. Samia pia kama kiongozi mwenye kuguswa na kuyatafutia suluhu matatizo ya wananchi wake, akieleza namna ambavyo pia alisikia na kuondoa misururu ya kodi, ubambikizaji wa tozo na kodi pamoja na mahusiano mabaya ya mamlaka ya mapato TRA katika ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara.
"Mhe. Mgombea mara baada ya kupata manung'uniko hayo kodi na tozo zaidi ya 250 alizifuta ili kuwapa nafuu watanzania. Alikuta pia madeni mengi serikali ikidaiwa, nayo alilipa yote ili kuwapa nafuu Watanzania, Amejenga hospitali, amenunua mashine za CT- Scan na mambo mengine mengi kila kona ya Tanzania." Amesema Mwigulu.
Dkt. Mwigulu Nchemba pia amesema mambo hayo aliyoyafanya Dkt. Samia kwa kipindi kifupi yametambulika pia kimataifa kwa Taasisi zote kubwa zinazopima maendeleo bora ya kiuchumi na ustawi wa jamii, akisema chini ya Dkt. Samia Tanzania imetajwa na Benki ya dunia mara kadhaa kama kinara katika sekta za maji, elimu na afya kwa kutimiza malengo ya milenia, akiwasihi watanzania kuwakataa wale wote wanaomshambulia Dkt. Samia kwani dhamira ya watu hao ni kudhohofisha maendeleo ya wananchi.





No comments:
Post a Comment