KAMPENI ZA DKT. SAMIA KUBISHA HODI MKOANI GEITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, October 12, 2025

KAMPENI ZA DKT. SAMIA KUBISHA HODI MKOANI GEITA



Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumapili Oktoba 12, 2025 anaanza Ziara yake ya Kampeni Mkoani Geita, akitarajiwa kuwa na Mikutano ya Kampeni Bukombe, Masumbwe na Runzewe- atakapozungumza na wananchi, kuomba kura na kuwaeleza utekelezaji wa ahadi na Ilani ya mwaka 2020/2025.

Dkt. Samia anaingia Katika Mkoa huo akiwa na msururu wa mafanikio katika Miaka yake minne ya uongozi ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Bukombe, Chato, Geita, Geita Manispaa, Mbogwe na Nyang'hwale, kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 83 hadi 91 pamoja na kupunguza vifo vya mama wajawazito kutoka 301 hadi vifo 234 na kupunguza maambukizi ya Ukimwi kutoka asilimia 5.1 hadi 4.90.

Dkt. Samia pia na serikali yake ya awamu ya sita wameendeleza pia mpango wa elimu bila ada kwa elimu ya kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita kwa kuongeza fedha za kugharamia mpango huo kutoka shilingi 14,251,970,197.84 hadi Shilingi 43,146,475,912.00 pamoja na kuongeza shule za msingi kutoka 581 hadi 757 na shule za sekondari kutoka 130 za awali hadi kufikia shule 245.

Serikali ya awamu ya sita wakati huu pia inaendelea na ujenzi wa soko la samaki katika Halmashauri ya Chato, ujenzi wa mradi wa chuo cha viumbe hai Chato kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.7, ujenzi wa miundombinu ya kituo cha mabasi Chato na Bwanga yenye kugharimu shilingi Bilioni 14, kuendelea na ujenzi wa kituo cha mabasi na Soko Bukombe kwa gharama ya shilingi Bilioni 22, Ujenzi Kituo cha mabasi Nyang'hwale kwa gharama ya Milioni 608 na ujenzi wa uwanja wa mpira wa Magogo katika manispaa ya Geita mradi utakaogharimu jumla ya shilingi Bilioni 2.2.

Katika kuendelea kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, Ilani ya CCM inayonadiwa na Dkt. Samia imeahidi ndani ya miaka mitano ijayo kujenga Hospitali za Wilaya za Bukombe (Uyovu), Geita DC (Nyarugusu) na Chato (Bwanga), Kuongeza vituo vya afya kutoka 44 hadi 61, kuongeza Zahanati kutoka 215 hadi 271, Kuongeza Vijiji vyenye huduma ya maji safi kutoka 351 hadi 420, kujenga Vyuo 7 vya ufundi, kuanzisha maeneo ya uendelezaji wa bunifu na teknolojia (Innovation hubs) pamoja na kujenga Chuo Kikuu Wilayani Geita Mkoani humo.

No comments:

Post a Comment