
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Kihongosi, amesema kuwa tangu kuanza kwa kampeni za Urais kupitia CCM kwa mgombea wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zaidi ya wananchi milioni 45 tayari wameshiriki kwa namna mbalimbali.
Amesema kati ya hao, wananchi milioni 14.6 wamehudhuria mikutano ya kampeni, huku milioni 31.6 wakifuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii — jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kampeni za mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Oktoba 5, 2025) katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Kuu ya CCM, Dodoma, Kihongosi amesema uzinduzi wa kampeni uliofanyika kwa kishindo Agosti 28, 2025, katika Uwanja wa Kawe, Dar es Salaam, uliweka historia kwa kuvunja rekodi ya mahudhurio na shamrashamra tangu kuanzishwa kwa chama hicho.
Akiwasilisha takwimu za kampeni, Kihongosi ameeleza kuwa hadi sasa Dkt. Samia amefanya jumla ya mikutano 77 katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo Kanda ya Kati, Magharibi, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pwani, Pemba na Unguja.
Amesema wananchi wameendelea kuonesha imani kubwa kwa Dkt. Samia kwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025–2030), sera na ahadi zake.
Kihongosi amebainisha kuwa imani hiyo imechochewa na uongozi wenye mafanikio makubwa uliooneshwa na Dkt. Samia katika kipindi cha miaka minne, mafanikio yaliyowapa Watanzania matumaini ya taifa lenye maendeleo, mshikamano na ustawi wa watu wote.
Aidha, amesema kampeni hizo zimekuwa za kistaarabu, hazijajikita katika siasa za matusi au kejeli, bali zimebeba ujumbe wa matumaini, mshikamano na maendeleo jumuishi ya taifa.
Ameongeza kuwa kuanzia Oktoba 7, 2025, mgombea huyo ataendelea na ziara zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Simiyu, Mwanza na Mara, ambapo atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, kuwasilisha sera na kuelezea kwa kina dhamira ya CCM ya kuijenga Tanzania ya kisasa na yenye ustawi wa kiuchumi.
“Tunawaomba wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo, wakimsikiliza mgombea wetu ambaye amejidhihirisha kuwa ni kiongozi mwenye dira, busara na uwezo wa kuyaongoza mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wote,” alisisitiza Kihongosi.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa CCM itaendelea kuendesha kampeni zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku ikihimiza amani, umoja na mshikamano wa kitaifa katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi.
No comments:
Post a Comment