
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Oktoba 11, 2025 anaanza Mikutano yake ya Kampeni Mkoani Shinyanga, akinadi ilani ya Chama chake, kuomba kura za ushindi pamoja na kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa Miaka minne aliyoongoza serikali ya awamu ya sita, akiatarajiwa kuwa na Mikutano kwenye Wilaya za Kahama na Shinyanga.
Dkt. Samia anaingia Mkoani Shinyanga akitokea Mkoa wa Simiyu jana Oktoba 10, 2025, akijivunia utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo Mkoani humo ikiwa ni pamoja na Maboresho ya Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Kukamilika kwa Kituo cha afya Kinaga, kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi kutoka asilimia 63 hadi 79 kwa Kahama Manispaa pamoja na kuendeleza utekelezaji wa mradi wa maji wa Ziwa Viktoria katika Vijiji vya Kahama na kuanzisha soko la Kimataifa na mazao Mjini Kahama.
Katika Miaka minne ya Dkt. Samia madarakani kando ya kuendelea kuziendeleza tunu za Taifa ikiwemo amani na usalama na uhuru wa Tanzania, Dkt. Samia amefanikisha pia kukamilisha ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa Vituo viwili vya afya Ng'wanhalanga na Lagana pamoja na skimu kadhaa za umwagiliaji.
Kwa Ushetu katika msururu wa mafanikio, serikali ya Dkt. Samia imefanikisha ujenzi wa shule mpya kumi za mkondo mmoja na madarasa 270, uendelezaji wa majengo nane ya Hospitali ya Wilaya, ujenzi wa mejengo 7 kituo cha afya ya OPD, maabara, Theatre, pamoja na mochwari huku Ushetu wakifanikiwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na Vituo 3 vya afya vya Igwamanoni, Ulowa na Nyalwelwe.
Katika Ilani ya 2025/30 CCM wameahidi ujenzi wa mtandao wa maji kwenda Izuga na Kilango Wilaya ya Kahama, ujenzi wa soko la bidhaa za kilimo la Sango na Zongomera ikijumuisha Vibanda vya maduka 184 na Vizimba 200, huku kwa Wilaya ya Shinyanga wakiahidi ujenzi wa jengo la mama na mtoto Hospitali ya rufaa ya Mkoa, ujenzi wa shule 5 mpya za msingi, ujenzi wa chuo cha mafunzo ya ufundi VETA kando ya mengine mengi yakihusu sekta mbalimbali za kijamii na uchumi ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara.
No comments:
Post a Comment