
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Kaimu Meneja wa Ukaguzi wa Madini na Huduma za Maabara kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Mwarabu Mvunilwa, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Maabara ya Tume ya Madini mwaka 2020, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Sekta ya Madini, ikiwemo kuongezeka kwa uhakika wa shughuli za uchimbaji, biashara na usafirishaji wa madini, pamoja na kuimarika kwa makusanyo ya maduhuli ya Serikali mwaka hadi mwaka.
Akizungumza leo, Oktoba 23, 2025, katika ofisi za maabara hiyo zilizopo Msasani, jijini Dar es Salaam, wakati wa maandalizi ya kipindi maalum kinachoandaliwa na Clouds Media Group, Mhandisi Mvunilwa amesema maabara hiyo imekuwa chachu kubwa katika kukuza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa.
“Tangu kuanzishwa kwa maabara hii, tumeona mafanikio makubwa. Wafanyabiashara wengi sasa wanafanya shughuli zao kwa uhakika zaidi kutokana na huduma za uhakiki wa madini zinazotolewa kwa viwango vya kimataifa. Hii imechangia ongezeko la mapato ya Serikali na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hii,” amesema Mhandisi Mvunilwa.
Ameongeza kuwa maabara hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wa madini wanaosafirisha madini nje ya nchi kupitia Bandari ya Dar es Salaam, kutokana na ukaribu wa maabara na lango hilo kuu la biashara.
“Wafanyabiashara hupata unafuu mkubwa kwa kuwa huduma za upimaji wa madini zinapatikana karibu na bandari. Pia wawekezaji huleta sampuli mbalimbali kwa ajili ya vipimo na ushauri wa kitaalam kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji,” amefafanua.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mvunilwa, maabara hiyo imejipatia umaarufu kimataifa kutokana na ubora wa huduma zake, ikibeba wataalam waliobobea na vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kupima aina zote za madini kwa muda mfupi na kwa usahihi wa hali ya juu.
“Tumeendelea kuwa kivutio kwa nchi jirani ambazo zinakuja kujifunza kutoka kwetu. Hii ni ishara kuwa Tanzania inazidi kuwa kinara katika upimaji na uthibitisho wa ubora wa madini katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema.
Akizungumzia mikakati ya baadaye, Mhandisi Mvunilwa amesema Tume kupitia maabara hiyo imepanga kusogeza huduma zake karibu zaidi na maeneo yenye shughuli kubwa za uchimbaji wa madini nchini, ili kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara kupata huduma kwa urahisi zaidi.
Aidha, amewataka wadau wa sekta ya madini kutumia maabara hiyo ambayo inatoa huduma bora kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyotambulika kimataifa.
Kwa upande wake, Salustian Raymond, mfanyabiashara wa madini ya kinywe, amesema maabara hiyo imekuwa msaada mkubwa kwao kwa kutoa huduma za haraka na zenye ubora wa juu.
“Maabara hii imerahisisha biashara kwa kiasi kikubwa. Tunashukuru kwa huduma bora tunazopata kutoka kwa wataalam waliobobea chini ya uongozi wa Mhandisi Mvunilwa. Gharama ni nafuu na zinamwezesha kila mwenye nia njema kuwekeza katika sekta ya madini,” amesema Raymond.




No comments:
Post a Comment