
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na viongozi wa nchi za India, China, Mauritius na Comoro kwenye sherehe za kumuapisha Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Patrick Herminie zilizofanyika kwenye Uwanja wa Umoja, jijini Victoria nchini humo.
Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwa miongoni mwa viongozi hao wakuu wakiwemo Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na viongozi wa juu kutoka vyama rafiki vya siasa. Rais Herminie aliapishwa jana (Jumapili, Oktoba 26, 2025) kuwa Rais wa sita wa nchi hiyo.
Viongozi hao ni Makamu wa Rais wa India, Bw. Chandrapuram Ponnusamy Radhakrishnan; Waziri Mkuu wa Mauritius, Dkt. Navinchandra Ramgoolam; Makamu wa Rais wa Chama cha Chinese People’s Political Consultative Conference (CPPCC) Bw. Gao Yunlong na Rais wa Baraza la Mawaziri la Kamisheni ya Bahari ya Hindi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Bw. Mohamed Mbae.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Cosato Chumi; Balozi wa Tanzania nchini Kenya anayeiwakilisha Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Bernard Kibesse na maafisa waandamizi wa Serikali.
Ushindi wa Rais Herminie, umekiondoa chama kilichokuwa madarakani cha Linyon Demokratik Seselwa (LDS) ambacho kilishinda uchaguzi wa mwaka 2020. Rais Herminie ambaye mwaka huu aligombea nafasi ya urais kupitia Chama cha United Seychelles (US) aliapishwa jana baada ya kupata asilimia 52.7 ya kura zilizopigwa na kumshinda mpinzani wake, Bw. Wavel Ramkalawan wa chama cha LDS aliyepata asilimia 47.3 ya kura zote kwenye duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 11, 2025. Katika duru ya kwanza iliyofanyika Septemba 27, mwaka huu hakuna mgombea urais aliyezidi asilimia 50 ya kura zote baina ya wagombea sita wa urais.
Katika sherehe hizo, Rais Dkt. Herminie alikula kiapo kwanza cha utii kwa wananchi mnamo saa 12.35 jioni na kisha akala kiapo cha urais saa 12.37 na kutia saini hati hizo mbele ya Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Rony Govinden.
Akilihutubia Taifa hilo mara baada ya kuapishwa, Rais Dkt. Herminie alisema anakubali kupokea dhamana aliyopewa na wananchi wa Shelisheli kwa kuwa anatambua wajibu mkubwa unaotokana na Ilani ya chama chao isemayo: “Kwa ajili ya wengi, na siyo wachache."
Rais huyo alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wake kuwa wasitarajie kuwa mambo yote yatafanyika ndani ya siku moja. “Ninaongea kwa dhati kuwa mambo yote hayawezi kukamilika ndani ya siku moja. Lakini kuanzia leo tutaanza kazi, tutayapa kipaumbele masuala yote ya muhimu yanayogusa maisha ya wananchi na kwa msingi huo, Serikali yangu imeanzisha “Siku 100 za Kwanza - Mkataba wa Kijamii na Watu wa Shelisheli.”
Katika hotuba yake iliyodumu kwa dakika 17, Rais Dkt. Herminie aliiomba jumuiya ya kimataifa iungane na nchi hiyo kujenga urafiki na mshikamano. “Tunataka tushirikiane, tukue pamoja, tufanye biashara kwa usawa, tunakaribisha uwekezaji na ubadilishanaji wa maarifa ambao utanufaisha pande zote mbili,” alisisitiza.
Pia Rais Herminie alisisitiza kwamba Serikali yake italibeba kwa dhati suala la vijana na siyo kulizungumzia tu kwenye majukwaa. “Ninyi vijana siyo kwamba mnapaswa kusubiri fursa zijazo, ninyi mpo hapa katikati yetu; ninyi ni viongozi wa kesho. Ninawasihi vijana wa Kishelisheli mjikite kwenye masuala ya ubunifu, sayansi, teknolojia na akili unde kama hamtaki kuachwa kwenye hii dunia inayoenda kwa kasi. Tutaijenga nchi yetu kwa pamoja na hatutaacha vipaji vyenu vipotee wala ndoto zenu zipepee zikiacha nchi yetu tupu,” alisisitiza.
Dkt. Herminie aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Seychelles kuanzia mwaka 2007 hadi 2016 na kabla ya hapo, alikuwa kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni kuanzia mwaka 1998 hadi 2003.
Kabla ya kuondoka uwanjani, Rais Dkt. Herminie alishuhudia nyimbo mbalimbali, mashairi na fashfash ya mafataki iliyodumu kwa zaidi ya dakika 5.

No comments:
Post a Comment