MATIVILA AAGIZA MKANDARASI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 15, 2025

MATIVILA AAGIZA MKANDARASI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA



Na Mwandishi Wetu, Rufiji, Pwani


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amemtaka Mkandarasi JUIN Company Ltd anayekarabati barabara ya Nyamwage-Tawi-Kikobo yenye urefu wa Kilomita 56 kwa kiwango cha changarawe wilayani Rufiji mkoani Pwani, kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Mhandisi Mativila ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa barabara hiyo ya Nyamwage-Tawi-Kikobo ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 35.

"Mradi huu umechelewa na mvua zinakuja, kwa hali ilivyo mvua zikianza kunyesha kazi zitakuwa hazifanyiki, ninachosisitiza kabla mvua hazijanyesha Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana ili kazi ikamilike kwa wakati, pia naomba TARURA msimamie kwa ukaribu ili barabara hii iweze kupitika”, amesema.

Aidha, Mhandisi Mativila amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha za bajeti ya TARURA kutoka Shilingi Bilioni 275 hadi Shilingi Bilioni 700 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara za wilaya ili ziweze kusaidia shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa amesema wamejipanga kuhakikisha utekelezaji wa kazi zote zinazoendelea za mwaka wa fedha 2024/25 utekelezaji wake unakamilika ambapo ametoa wito kwa Makandarasi wote wanaotekeleza kazi za TARURA mkoa wa Pwani hasa wale ambao wamekuwa wakichelewesha kazi warudi “site” ili kukamilisha kazi hizo.

“Tunawaomba Makandarasi kufanya kazi kama mikataba inavyowataka kwasababu vinginevyo tunaweza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yao, hatuwezi kuvumilia kazi zimekuwa hazifanyiki kwa wakati, sisi tutakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha tunasimamia kwa ukaribu kazi hizo kama Naibu Katibu Mkuu alivyotuelekeza”, amesema.

Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa TARURA wilaya ya Rufiji, Mhandisi Nicholaus Ludigery amesema kuwa mradi huo upo katika awamu mbili ambapo ni ukarabati wa barabara ya Nyamwage-Tawi Km 28 kwa kiwango cha changarawe kwa thamani ya Shilingi 1,163,543,000 utekelezaji umefikia asilimia 35 pamoja na ukarabati wa barabara ya Nyamwage-Tawi-Kikobo kwa thamani ya shilingi 998,780,000 utekelezaji umefikia asilimia 5.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo itasaidia kuzifikia huduma za kijamii kama elimu na afya na pia kuchochea shughuli za kiuchumi kama biashara na kilimo kwani wananchi wa maeneo hayo wanajishughulisha na kilimo cha korosho, ufuta, machungwa, mihogo na minazi ambapo barabara hiyo itawasaidia kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja na wilaya ya Rufiji kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment