MKOMI AHIMIZA UWAZI NA UWAJIBIKAJI KUPITIA MIFUMO YA TEHAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 9, 2025

MKOMI AHIMIZA UWAZI NA UWAJIBIKAJI KUPITIA MIFUMO YA TEHAMA



Na MWANDISHI WETU, OKULY BLOG, DODOMA


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi, amewasisitiza Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa utumishi wa umma, ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi (PEPMIS) na Mfumo wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Miradi (PIMS).

Bw. Mkomi alitoa wito huo leo Oktoba 09, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Tatu cha Baraza la Nane la Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria, kinachofanyika kwa siku mbili.

Amesema watumishi watakaoshindwa kutimiza matakwa ya matumizi ya mifumo hiyo hawatastahili kupandishwa vyeo, huku akibainisha kuwa matumizi sahihi ya mifumo hiyo yatasaidia kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Najua ni mfumo mgeni na wengi wetu hatuupendi kwa sababu unakuja kutubana, lakini niwahamasishe kwamba mifumo hii imeletwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi,” amesema Mkomi.

Aidha, ameeleza kuwa uanzishwaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika sehemu za kazi ni utekelezaji wa haki ya ushirikishwaji wa wafanyakazi, lengo likiwa ni kuboresha maslahi na mahusiano bora kati ya waajiri na wafanyakazi.

Ameongeza kuwa uanzishwaji wa mabaraza hayo ni utekelezaji wa Kifungu cha 74(1), (2) na (3) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366, pamoja na Kanuni ya 107 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022.

“Baraza hili ni jukwaa muhimu mahali pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na wafanyakazi wake. Ni matumaini yangu kuwa jukwaa hili litatumika kuishauri Wizara katika kusimamia maslahi, haki na ustawi wa wafanyakazi,” alisisitiza Mkomi.

Kikao hicho pia kimepangwa kujadili utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2024/2025, pamoja na kupitia mafanikio ya Wizara na taarifa ya bajeti ya mwaka 2025/2026.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu, Bw. Mkomi aliwahimiza watumishi kujitokeza kwa wingi kushiriki kupiga kura.

“Mimi sina chama, lakini nina mapenzi na watu fulani. Niwahimize watumishi wenzangu kushiriki kwenye uchaguzi kwa kujitokeza kupiga kura. Wanasiasa wanahamasisha wananchi, nasi watumishi tuwe mfano mzuri,” alisema.

Kuhusu Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, Mkomi alisema anaamini wajumbe wa baraza hilo watajadili namna bora ya kuboresha utendaji wa kitengo hicho ambacho kinahudumia wananchi wengi wanaotafuta suluhu za matatizo yao ya kisheria.

“Niwaombe wenzetu wanaosimamia kitengo hiki waendelee kukisimamia kwa ukaribu ili tuone matokeo chanya yanayotarajiwa,” aliongeza.


Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, amesema lengo kuu la kikao hicho ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji na utekelezaji wa mipango ya Wizara pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.









No comments:

Post a Comment