
Nachingwea, Lindi
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE programu ya uondoaji vikwazo katika barabara (Bottleneck) umekamilisha matengenezo ya eneo korofi lenye urefu wa kilomita 2 katika barabara ya Mnero-Miembeni- Chikoko wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Akiongea katika mahojiano maalum, Meneja wa TARURA Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Sumbuko Kyamba amesema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 30.88 ilikuwa na sehemu korofi yenye urefu wa kilomita 2 ambapo hadi sasa matengenezo yake yamekamilika.
"Barabara hii ilikuwa haipitiki hasa kipindi cha masika kwa sababu hiyo tuliamua kuipa kipaumbele kupitia mradi wa RISE ili itengenezwe na kutoa huduma kwa wananchi", amesema Mhandisi Sumbuko.
Naye, Bi. Hadija Omary mkazi wa Mnero amesema kuwa shughuli za kijamii na kiuchumi kwasasa zinaenda vizuri huku akiipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya ujenzi wa barabara.
Bw. Said Mpinga mkazi wa Chikoko amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo umewasaidia kusafirisha mazao pia wanafunzi wanaweza kwenda shule kwa urahisi.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE programu ya uondoaji vikwazo katika barabara inaendelea na zoezi la uondoaji vikwazo barabarani katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma kwa urahisi.




No comments:
Post a Comment