DKT. SAMIA AMETOA BILIONI 200 KUJENGA MFUMO MPYA WA MAJITAKA ILALA- ZUNGU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 22, 2025

DKT. SAMIA AMETOA BILIONI 200 KUJENGA MFUMO MPYA WA MAJITAKA ILALA- ZUNGU


Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mgombea Urais wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imetoa jumla ya shilingi Bilioni 200 kwaajili ya usimikaji wa miundombinu mipya ya Majitaka ndani ya Jiji la Ilala ili kuzuia majitaka hayo kuelekezwa baharini kama ambavyo ilikuwa awali.

Kauli hiyo iliyoambatana na shukrani kwa Dkt. Samia imetolewa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilala kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu wakati wa Mkutano wa Kampeni za Dkt. Samia leo Jumanne Oktoba 22, 2025 Kinyerezi, Ilala Dar Es Salaam kwenye Viwanja vya Kecha, akisema Dkt. Samia ameamuru majitaka hayo kutoelekezwa baharini ili kulinda uhai wa viumbe maji wa baharini wakiwemo samaki.

Kulingana na Zungu, tayari mkandarasi yupo kwenye eneo la kazi akiweka miundombinu mipya ya Majitaka kutoka Gymkhana, Malick road, Upanga, Jangwani Sekondari, Mchikichini mpaka buguruni, lengo likiwa ni kuliweka Jiji hilo pia katika hadhi sahihi sambamba na kuyatumia maji taka hayo kwaajili ya kilimo mara baada ya kuwa yamesafishwa.

Zungu pia amezungumzia changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama katika baadhi ya maeneo ya Ilala, akisema chanzo cha tatizo hilo imekuwa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Mkoani Dar Es Salaam, akiwaomba wananchi wa Kivule, Ukonga, Segerea, Ilala na Kinondoni kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki kifupi cha utatuzi wake.

"Tukubali kero hii lakini nina habari njema DAWASA chini ya Aweso usiku na mchana wanahangaika kuhakikisha maji yanarudi na Niipongeze DAWASA kwa namna wanavyojitoa kuhakikisha kero hii inaisha. Nawaomba watu wa Kariakoo, Upanga, Kisutu, Kivukoni, Ilala, Jangwani na Mchikichini, Maji yameanza kutoka, tuwe na uvumilivu." Amesema Mhe. Zungu.

Katika hatua nyingine Zungu amemshukuru Dkt. Samia kwa kuamua kuuendeleza mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar Es Salaam maarufu kama DMDP, akisema mradi huo umekuwa chachu ya ujenzi wa miundombinu katika Jimbo na Wilaya ya Ilala.

No comments:

Post a Comment