RAS ARUSHA: MAFUNZO YA PPRA YATAONDOA UWEZEKANO WA KUPATA HASARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 22, 2025

RAS ARUSHA: MAFUNZO YA PPRA YATAONDOA UWEZEKANO WA KUPATA HASARA


Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Missaile Musa amesema mafunzo yanayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) yataondoa uwezekano wa Serikali kupata hasara kwenye michakato ya ununuzi wa umma na kufanikisha juhudi za kuwaletea maendeleo watanzania.

Ameyasema hayo Oktoba 20, 2025 jijini Arusha kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo, Bw. Mosses Pesha alipokuwa akifungua mafunzo ya siku sita kuhusu matumizi ya moduli mpya ya Usimamizi wa Mikataba kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki – NeST, pamoja na mabadiliko ya bei katika mikataba iliyoingiwa (price adjustment indices). Mafunzo hayo yanatolewa na Mamlaka hiyo kwa watendaji wa Serikali takribani mia tatu kuanzia Oktoba 20 – 25, 2025. 

“Pamoja na mafunzo ya NeST, mtajifunza pia kuhusu mabadiliko ya bei katika mikataba iliyoingiwa (price adjustment indices). Kujua jinsi ya kufanya mabadiliko ya bei katika mikataba iliyoingiwa ni muhimu sana, kwani yasipofanyika kwa usahihi yanaweza kusababisha hasara kubwa kwa Serikali,” alisema. 

Alisema kuanza kutumika kwa moduli ya usimamizi wa mikataba kupitia Mfumo wa NeST ni hatua kubwa inayotekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutumia mifumo ya TEHAMA kudhibiti ubadhirifu na kuongeza ufanisi. 

“Matumizi ya moduli hii ya usimamizi wa mikataba yatasaidia sana kudhibiti ongezeko la gharama. Pia, itasaidia kuhakikisha ubora na muda wa utekelezaji wa mikataba,” alisema. 

Awali, Mkurugenzi wa Kuendeleza Uwezo wa Ununuzi wa Umma kutoka PPRA, Bi. Winnifrida Samba alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza ufanisi kwa watendaji hao kutumia moduli mpya ya usimamizi wa mikataba kupitia Mfumo wa NeST, ambayo imeanza kutumika kikamilifu kwa taasisi za umma thelathini. 

Mwenyekiti wa chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania, Dkt. Emmanuel Urembo aliyehudhuria mafunzo hayo, amesema moduli ya usimamizi wa mikataba kupitia Mfumo wa NeST ni mwarobaini wa changamoto nyingi zilizokuwa zikijitokeza kwenye michakato ya ununuzi wa umma. 

Tangu kuanzishwa kwake Julai 1, 2023, PPRA kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali, imejenga moduli tatu za Mfumo wa NeST ambazo ni moduli ya usajili (e-registration), moduli ya michakato ya zabuni (e-tendering) na moduli ya usimamizi wa mikataba (e-contract management).

Mamlaka hiyo inaendelea na ujenzi wa moduli zilizosalia kwenye Mfumo wa NeST, ambazo ni malipo (e-payment), masoko (e-marketing) na mnada (e-auction).

No comments:

Post a Comment