
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tarehe 9 Oktoba, 2025 wametoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Nyangaka, iliyopo Halmashauri ya Bariadi Mji pamoja na kuhamasisha kuhusu matumizi sahihi ya nishati ya umeme shule hapo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo; Bi. Jaina Msuya, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi, amesema nishati safi ya kupikia ni dhana inayotumika kuelezea na kubainisha nishati na teknolojia sahihi ambapo kwa pamoja hutoa moshi wenye kiwango kidogo cha sumu pale zinapotumika kwa usahihi.
“Nishati safi ya kupikia hupimwa kwa ufanisi katika muda mfupi, urahisi wa kutumia, upatikanaji, usalama, unafuu (Bei ya matumizi kila siku) na isiyowaweka Watumiaji katika mazingira hatarishi na yenye sumu” ameeleza Bi. Jaina.
Ametolea mfano matumizi ya majiko ya umeme, gesi pamoja na majiko banifu yanayotumia mkaa na kuni mbadala pamoja kuni na mkaa kidogo na kuongeza kuwa teknolojia hizo zinapatikana ingawa zinahitaji kiwango kikubwa cha fedha ya kununua.
“Licha ya gharama ya kununulia teknolojia za nishati safi kuwa juu mfano jiko la umeme la ‘induction’ lakini ukiwa na jiko hili, unatumia chini ya uniti moja ya umeme ambayo kwa bei ya TANESCO (Mjini inauzwa shilingi 356.24) na (Kijijini inauzwa shilingi 122); unakuwa umepika na kuivisha chakula, wakati huu kopo la mkaa ni zaidi ya shilingi 1,000 na utahitaji kununua zaidi ya kopo moja kwa ajili ya kupika chakula cha siku moja kwa familia ya watu watatu,”amesema Bi. Jaina.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shula ya Msingi Nyangaka Bi. Theresia Chuwa ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo hayo ya vitendo kwa Wanafunzi wa shule hiyo na kuongeza kuwa yametoa fursa ya Wanafunzi kujifunza na watayakumbuka kwa kuwa yametolewa kwa vitengo.
“Tunashukuru kwa kuwa mchakato wa kujifunza unachukua muda na ni Imani yetu, kuwa Wanafunzi wamepata kitu na wataendelea kujifunza na kuwa Mabalozi wa kesho wa nishati safi ya kupikia kwenye jamii na familia zao” amesema Mwalimu Theresia.




No comments:
Post a Comment