
Mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Pangani Mkoani Tanga na Waziri wa Maji wa serikali ya awamu ya sita Mhe. Jumaa Aweso, amesema katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan jumla ya shilingi Trilioni tatu zimetolewa ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama yanawafikia wananchi wote nchini.
Aweso amebainisha hayo mbele ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania, wakati wa Mkutano wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi Wilayani Kinondoni Mkoani Dar Es Salaam kwenye Viwanja vya Leaders Club leo Oktoba 21, 2025, akisema kati ya fedha hizo Shilingi Trilioni 1 Dkt. Samia alielekeza ziende Dar Es Salaam na kufanikisha kuondoa changamoto ya Maji, iliyokua ikiathiri Mkoa huo katika miezi ya Septemba, Oktoba na Novemba ya kila mwaka.
Kulingana na Waziri Aweso, Changamoto za maji Dar Es Salaam zilisababishwa na utegemezi wake kwenye chanzo kimoja cha maji cha Mto Ruvu na kutokana na mabadiliko ya tabianchi mto huo ulikuwa ukikauka msimu wa kiangazi na hivyo kusababisha adha ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa Mkoa huo.
Katika utatuzi wa changamoto hiyo, Dkt. Samia aliidhinisha utoaji wa fedha za dharura shilingi Bilioni 21 kwaajili ya kufufua visima vya Maji vya Kimbiji na kisha kutoa Maji Wilayani Kigamboni na kuyapeleka katikati ya Jiji ili kuhudumia wananchi wa eneo lote la katikati ya Jiji la Dar Es Salaam.
Aidha Aweso pia amemshukuru Dkt. Samia kwa uwekezaji wake kwenye mifumo ya majitaka Mkoani Dar Es Salaam ambapo jumla ya shilingi Bilioni 400 zimetumika katika kipindi cha miaka minne pekee ya Uongozi wa awamu ya sita wa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ni Oktoba 29, 2025 na Dkt. Samia anaomba ridhaa kwa watanzania ili kuendeleza zaidi kazi aliyoianza miaka minne iliyopita katika kulinda, kustawisha na kuheshimisha utu wa Mtanzania kupitia huduma bora na za karibu zaidi katika sekta za afya, elimu, maji na huduma nyingine muhimu za kijamii na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment