
Na Okuly Julius - OKULY BLOG DODOMA
Tume ya Utumishi wa Umma imepokea jumla ya rufaa na malalamiko 108 kutoka kwa watumishi wa umma nchini, ambapo makosa yanayoongoza ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma, utoro kazini, kughushi vyeti, kutoa taarifa za uongo, uzembe kazini na wizi wa mali za umma.
Akitoa taarifa Mbele ya Waandishi wa habari leo Oktoba 20,2025 jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu wa Tume hiyo, Bw. John Mbisso, kufuatia mkutano wa kwanza wa mwaka wa fedha 2025/26 wa tume hiyo uliofanyika kuanzia, tarehe 29 Septemba hadi 17 Oktoba 2025 chini ya Mwenyekiti Jaji Mstaafu Hamisi Kalombola, ameeleza kuwa tume hiyo ilijadili na kufanya maamuzi juu ya rufaa na malalamiko hayo yaliyowasilishwa na watumishi kutoka kada mbalimbali.
Bw. Mbisso, amefafanua kuwa kati ya rufaa 93 zilizowasilishwa,Rufaa 34 zimekubaliwa bila masharti,Rufaa 9 zimekubaliwa kwa masharti ya kuanza upya kwa mamlaka za nidhamu husika,Rufaa 38 zimekataliwa ,Rufaa 10 zilitupiliwa mbali kwa sababu ziliwasilishwa nje ya muda wa kisheria,Kuhusu malalamiko 15 yaliyowasilishwa,
Bw. Mbisso ameeleza kuwa Malalamiko 6 yalikubaliwa,Malalamiko 6 yakakataliwa,Malalamiko 3 yalitupiliwa mbali
Aidha, alibainisha kuwa kada zilizowasilisha rufaa na malalamiko kwa wingi ni kutoka mamlaka za serikali za mitaa.
Upande wa Malalamiko ya Watumishi, yaliyotajwa ni pamoja na kutolipwa stahiki zao na waajiri wao, ikiwemo mishahara, posho za uhamisho, na stahiki nyingine za kisheria.
Pia, watumishi walilalamikia kuchelewa kupandishwa vyeo na madaraja au kutopandishwa kabisa, pamoja na kuondolewa kazini kinyume cha sheria.
Bw. Mbisso amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili, sheria na taratibu za utumishi ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha Mbisso amesema Katika mkutano huo, warufani 18 na warufaniwa 3 walipewa nafasi ya kufika mbele ya tume kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zao za rufaa na majibu ya hoja hizo.
Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ufuatiliaji wa haki za watumishi wa umma kwa mujibu wa sheria, ili kuhakikisha utumishi wa umma unazingatia misingi ya uwazi, haki na uwajibikaji.


No comments:
Post a Comment