Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ikiwa Watanzania watampa ridhaa ya kuunda serikali, miongoni mwa mambo atakayoyafanya mapema ni pamoja na kupokea ripoti za Tume aliyoiunda ya Marekebisho ya mifumo ya kodi nchini na Tume mbili ya tathmini kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa eneo la Hifadhi la Ngorongoro Mkoani Arusha.
Tume nyingine ambayo itakabidhi ripoti yake kwa Dkt. Samia ni Tume ya tathmini ya utekelezaji wa uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha, akisema atachukua hatua stahiki kulingana na maoni ya wananchi na mapendekezo waliyoyaeleza kwa Tume hizo zilizochukua maoni yao.
Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumatano Oktoba 22, 2025 wakati wa Mkutano wake wa hadhara wa Kampeni kwenye Viwanja vya Kecha, Kinyerezi, Ilala Mkoani Dar Es Salaam, akisema Tume hizo zilishindwa kukabidhi ripoti zao licha ya kumaliza kazi yake kutokana na mwingiliano wa ratiba za Kampeni na uchaguzi Mkuu wa Tanzania.
Dkt. Samia pia ameeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye mabadiliko na mageuzi mbalimbali anayoyachukua ikiwemo kurejea kwa heshima ya Tanzania Kimataifa pamoja na kuimarisha mahusiano yake ya Kidiplomasia, suala ambalo limekuza heshima ya Tanzania Kimataifa.
Malengo ya Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi ilikuwa ni pamoja na kuchambua sera na sheria za kodi na kubaini maeneo ya kuboresha, kubaini athari za viwango vya kodi katika sekta ya uchumi, kufanya mapitio ya mifumo na mbinu za ukusanyaji wa mapato ya kodi na ya siyo ya kodi pamoja na kuchambua usimamizi na utekelezaji wa sheria za kodi na kuchambua mapato ya siyo ya kodi na namna yanavyoathiri sekta za uzalishaji.
Mengine ni kubainisha changamoto zinazoathiri utendaji wa mamlaka zinazosimamia ukusanyaji wa kodi, ushuru, tozo na ada mbalimbali, kuchambua usimamizi wa mapato ya mamlaka za udhibiti na serikali za mitaa, kupokea na ku chambua maoni na mapendekezo ya wananchi na wadau, kupata uzoefu kutoka kwenye nchi ningine kuhusu masuala ya kodi na kuandaa ripoti na mapendekezo jumuishi.
No comments:
Post a Comment