
Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la Benki Kuu Dodoma, Bw. Nolasco Maluli akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Meneja Msaidizi wa Uhusiano wa Umma Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Noves Moses akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.

Meneja msaidizi uchumi wa Benki Kuu Tawi la Dodoma. Bw. Shamy Chamicha akiwasilishamada katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vyombo vya habari nchini katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya uchumi na masoko ya fedha, hatua inayosaidia kuongeza uwazi wa kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Hayo yameelezwa leo Novemba 19, 2025 jijini Dodoma na Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la BoT Dodoma, Bw. Nolasco Maluli, wakati akifungua semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Zanzibar, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Bw. Maluli amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kutuma taarifa sahihi kwa umma kupitia habari, vipindi na makala za uchumi na fedha ambazo zimekuwa zikiwasaidia wananchi kuelewa mwenendo wa uchumi wa nchi.
Amesema waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya wataalamu wa uchumi na wananchi, na kwamba kukosekana kwa elimu sahihi kuhusu masuala ya fedha kunaweza kusababisha kupotosha umma au kupunguza imani ya wawekezaji katika masoko ya fedha nchini.
Bw. Maluli ameongeza kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yamelenga kuwawezesha wanahabari kufanya uchambuzi mpana na wa kitaalamu kuhusu masuala ya kifedha, ili kuongeza ubora wa taarifa wanazowasilisha kwa umma.
Amefafanua kuwa Benki Kuu ina mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza masoko ya fedha nchini kupitia ujenzi wa miundombinu wezeshi, usimamizi wa sheria, na uimarishaji wa nyenzo muhimu za masoko ya fedha.
Washiriki wa semina hiyo wanajifunza mada mbalimbali zikiwemo muundo na majukumu ya Benki Kuu, Sera ya Fedha inayotumia Riba ya Benki Kuu, elimu kuhusu hatifungani na umuhimu wake kwa taifa, elimu kuhusu huduma ndogo za fedha na usajili wa vikundi, pamoja na namna ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha kupitia mpango wa “Sema na BoT”.
Mada nyingine ni namna BoT inavyosimamia mifumo ya malipo nchini na utambuzi wa alama za usalama katika noti.



No comments:
Post a Comment