
Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) , Ramadhani Myonga, akiwasilisha mada ya namna ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha leo Novemba 20,2025 jijini Dodoma , wakati wa Semina kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na Benki hiyo.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha nchini, ikibainisha kuwa ulinzi huo ni nguzo muhimu katika uthabiti wa mifumo ya kifedha na usawa wa soko.
Akiwasilisha Mada ya namna ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha leo Novemba 20,2025 jijini Dodoma , wakati wa Semina kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na Benki hiyo , Afisa Sheria Mwandamizi kutoka BoT, Ramadhani Myonga, amesema ulinzi wa mteja ni mkusanyiko wa sheria, sera, taratibu na taasisi zinazolenga kuhakikisha haki za watumiaji zinalindwa, huku watoa huduma wakitakiwa kutoa bidhaa na huduma kwa uwazi, usahihi na bila mbinu za udanganyifu.
Myonga ameeleza kuwa Kanuni za BoT za mwaka 2019 kuhusu Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha ndizo zinazoratibu maeneo hayo, kwa kuhakikisha watumiaji wanpata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi ya kifedha.
Amebainisha kuwa maboresho katika kanuni na mifumo ya ulinzi wa watumiaji yanatokana na mafunzo yaliyopatikana kutokana na mgogoro wa kifedha wa mwaka 2007–2008, ambapo ilionekana kuwa upungufu wa ulinzi wa wateja nchini Marekani ulikuwa miongoni mwa sababu zilizoichochea dunia kukumbwa na mtikisiko mkubwa wa kifedha.
Akizungumzia hatua za kimataifa, Myonga alisema nchi mbalimbali zimeimarisha usimamizi wa masoko ya fedha kwa kupitisha sera na sheria mpya. Ametolea mfano Marekani, ambayo ilipitisha Sheria ya Dodd-Frank ya mwaka 2010 na kuanzisha mamlaka ya CFPB kwa ajili ya kulinda watumiaji wa huduma za kifedha, na Uingereza ambayo iliunda FCA mwaka 2012 kusimamia mwenendo wa soko na masuala ya haki za watumiaji.
Amesema hata mataifa mengi yanayoendelea, ikiwemo Zambia, yamefanya marekebisho ya sheria ili kuimarisha masharti ya ulinzi kwa wateja wa huduma za kifedha.
Myonga ameongeza kuwa Miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ulinzi wa Watumiaji imefanyiwa maboresho na sasa inajumuisha maeneo muhimu yanayotikisa sekta ya kifedha kama uwazi katika utoaji wa huduma, mwenendo wa biashara, ulinzi wa taarifa binafsi za wateja, elimu ya kifedha na utatuzi wa malalamiko. Amesema miongozo hiyo imekuwa nyenzo muhimu kwa nchi zinazoimarisha mifumo ya uwajibikaji katika sekta ya fedha.
Amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi wa watumiaji kwa kusimamia ubora na usalama wa taarifa, kudhibiti mwenendo wa watoa huduma, kuongeza uelewa wa kifedha kwa wananchi na kuhakikisha wateja wanapata huduma bila unyanyasaji, udanganyifu au mbinu zisizo za haki.
Kwa mujibu wa Myonga, hatua hizi zinalenga kuongeza imani ya umma katika sekta ya fedha, kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuhakikisha wananchi wanatumia huduma za kifedha kwa usalama, uaminifu na uelewa sahihi.


No comments:
Post a Comment