WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani vitekeleze sheria hizo bila upendeleo kwani tabia ya kuogopana na kuoneana aibu imechangia baadhi ya watu kukwepa wajibu wakati wengine wakibebeshwa mzigo wa sheria.
“Yeyote atakayevunja sheria akamatwe na hatua zichukuliwe kwa usawa. Huyu mmoja anavunja sheria anakamatwa, analipa. Huyu mwingine anavunja mbele yake anaachwa. Kama una haraka, toka mapema zaidi si kufidia kwa kuvunja sheria.”
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Novemba 26, 2025) wakati akifungua Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa haitakuwa uungwana kuona baadhi ya watu wakilipa adhabu papo hapo wanapokosea ilhali wengine wakiachwa kupita bila kuchukuliwa hatua.
Amewaonya baadhi ya viongozi na madereva wa Serikali ambao wanaelewa sheria vizuri lakini bado wanazikiuka kwa makusudi. “Ni muhimu kuwasaidia watumiaji wa vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji ambao kwa sehemu kubwa wanaweza kuwa hawazielewi sheria kikamilifu, badala ya kuwaadhibu kwa upendeleo.”
Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kuwapa Watanzania wote heshima na kuhakikisha sheria zilizowekwa zinatekelezwa kwa maslahi ya wote na kuongeza kuwa endapo zipo sheria ngumu kutekelezeka, basi zibadilishwe ili kila Mtanzania anufaike.
Ameviagiza vyombo vya usimamizi wa sheria vihakikishe kuwa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri wanazingatia usimamizi wa sheria na kuchukua hatua kwa yoyote anayevunja sheria akamatwe na kuchukuliwa hatua bila kuonewa aibu.
“Inaudhi mtu amebeba mgonjwa anafuata sheria, halafu mwingine anapita tu anavunja sheria, hapati adhabu. Mlalahoi akivunja sheria anapata adhabu, tunawapa kazi watekeleza sheria kuwaomba radhi watu waliovunja sheria. Naelekeza kila mtu afuate sheria, uwe wa serikalini ama uwe binafsi, tumeweka sheria, zifuatwe kama zilivyo.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema sekta ya uchukuzi ni mojawapo ya sekta wezeshi za uchumi duniani kota na kwamba watu wanahitaji njia za uchukuzi ili kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wa usafirishaji nchini ili kuhakikisha masuala ya nishati safi yanapewa kipaumbele. Akitoa mfano, Waziri Mbarawa alisema: “Uendeshaji wa reli ya kisasa (SGR) unatumia nishati ya umeme, mabasi ya mwendokasi njia ya Mbagala yanatumia gesi asili na baadhi ya taxi na bajaji zinatumia gesi asili.”





No comments:
Post a Comment