Na Eric Amani-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuchunguza na kufuatilia kwa kina ukiukwaji wa maadili kwa Viongozi wa Umma ili kuwa na taifa lenye uadilifu kwa ustawi wa taifa.
“Ninyi ndio wenye mamlaka ya kusema ukweli, fanyeni kazi iliyoanzisha chombo hiki, semeni ukweli bila kuogopa mtu wala kuonea mtu, chukueni hatua inapobainika kuna ukiukwaji wa maadili kwa yale yanayowahusu, shirikianeni na Taasisi simamizi za Maadili, ambayo hayawahusu pelekeni kwenye taasisi husika.”ameongeza Mhe. Kikwete.
Akiwa katika ziara ya kikazi leo katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi jijini Dodoma, Mhe. Kikwete amesema Serikali imelenga kupunguza mmomonyoko wa maadili katika taifa, hivyo Sekretarieti ya Maadili inao wajibu mkubwa kuhakikisha jambo hili linatekelezeka kwa ufasaha.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amewataka Viongozi wa Umma wote kuhakikisha wanakamilisha ujazaji wa Matamko kwa Njia ya Mtandao (ODS) kabla ya tarehe 31 Disemba na kuwasilisha kwa utaratibu uliopangwa.
Aidha, ameisisitiza Sekretarieti ya Maadili kuendelea kutoa elimu ya ujazaji wa ODS ili Viongozi waelewe kwa kina na kuwarahisishia katika ujazaji, na kuwataka wataalam wa TEHAMA kushughulikia changamoto za mfumo na kupokea maoni na mapendekezo ya kuboresha mfumo huo.
“Ukweli ni kuwa Dunia yetu imebadilika, tunaenda na Teknolojia, Kutokufahamu matumizi ya kompyuta isiwe kigezo cha kutojaza Matamko kwa Njia ya Mtandao,” ameongeza Mhe. Kikwete.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ameomba ushirikiano kwa taasisi hiyo ili waweze kutekeleza majukumu kwa umoja.
“Hongereni kwa kazi mnayoifanya, tumekuja kwa utambulisho, binafsi mimi ni mgeni kuliko Waziri wangu, kikubwa ninachohitaji kutoka kwenu ni ushirikiano katika kujifunza ili tuweze kufanya kazi yenye tija kwa taifa.” Mhe. Qwaray amesisitiza.
Akitoa neno la shukrani, Kamishna wa Maadili, Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi amemshukuru Waziri Kikwete pamoja Naibu Waziri kwa kuona umuhimu wa kwatembelea na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji.
“Mhe. Waziri tunashukuru kwa kututembelea, mimi pamoja na wenzangu tumepokea ushauri na maelekezo uliyotupatia, tunaahidi kuyafanyia kazi na kwenye changamoto tutakushirikisha.” ameongeza










No comments:
Post a Comment