DKT. MWIGULU: TANZANIA NI MALI YETU SOTE, SI MALI YA SERIKALI WALA CHAMA CHA SIASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 25, 2025

DKT. MWIGULU: TANZANIA NI MALI YETU SOTE, SI MALI YA SERIKALI WALA CHAMA CHA SIASA



WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania ni mali ya Watanzania wote wala si ya Serikali au chama cha siasa na hivyo kila mmoja anapaswa kuilinda.

“Tanzania si mali ya Serikali, Tanzania si mali ya chama cha siasa na vyama vya siasa vipo kwa sababu nchi ipo. Tuilinde nchi yetu. Mungu ametupa nchi nzuri na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo jioni (Jumanne, Novemba 25, 2025) wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali nchini katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema fedha zinazotumika kujenga miundombinu ya barabara, zahanati, vituo vya afya, miradi ya maji ni za Watanzania na wala si za Serikali. “Hakuna fedha ya Serikali kwenye miradi. Fedha yote inayotekeleza miradi ni yako Mtanzania isipokuwa inasimamiwa na Serikali.”

Amesema kila Mtanzania anachangia pato la Taifa na anajinyima aina fulani ya maisha ili kujenga barabara au zahanati kwenye eneo lake. “Ukinunua shati kuna sehemu unapeleka kujenga barabara, unakuwa umetenga sehemu ya kutumia na sehemu umejinyima ili kuchangia maendeleo ya nchi.”

Akielezea madhara ya vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu, Waziri Mkuu amesema vitendo vile vililenga kuhujumu uchumi wa nchi na vimesababisha uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo kuchoma ofisi za serikali 756; vituo vya mabasi ya mwendokasi 27; mabasi sita; nyumba za watu binafsi 273; vituo vya polisi 159; vituo vya mafuta 672; magari ya watu binafsi 1,642; pikipiki 2,268; magari ya serikali 976 zikiwemo ambulance.

Amesema maisha ya Mtanzania mmojammoja yanahusisha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kujipatia riziki zao. “Maisha ya Mtanzania ni ya kutoka eneo moja aende eneo jingine; haya si maisha ya Serikali, ni maisha ya Mtanzania mmoja mmoja. Maisha ya mwana Dar es Salaam ni kutoka hatua moja kwenda nyingine. Hakuna Mtanzania ambaye amejilimbikizia mali kwamba anaweza akakaa mwaka mzima bila kutoka. Atatoka Mbezi aende Posta, atatoka Kimara aende Kariakoo, atatoka Kariakoo aende Goba. Hawa watu wasipotoka unataka wale nini?”

Amesema uharibifu wa miundombinu uliofanyika ulilenga kuua uchumi wa nchi. “Kwamba mpango uliwekwa pasiwe na miundombinu ya hawa watu kusafiri. Je, watakula nini? Walipanga kuchoma stendi ya mabasi ya Magufuli, kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi na reli ya SGR. Hizi siyo mali za Serikali, ni mali za umma. Hivi unapochoma kituo cha DAWASCO kinachowapa maji safi na salama unataka hawa watu waishije?” alihoji Waziri Mkuu.

Dkt. Mwigulu amewasisitiza Watanzania wawe mstari wa mbele kuilinda Tanzania kwa kutoa taarifa pale wanapobaini watu wasiofahamika kwani hivi sasa hawafikii kwenye nyumba za kulala wageni.

“Niwaelekeze viongozi wa Serikali ngazi zote kuanzia wa mitaa, kitongoji na wa kijiji wawe macho; hawa watu wabaya wabaya hawafikii tena kwenye nyumba za wageni, wanafikia kwa mtu mmoja mmoja. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, kwa kujua kuwa huyo aliyemleta ni nani.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema wale wasioitakia mema Tanzania wanatamani mabaya zaidi yaendelee kutokea, hivyo ni busara kuwakataa kwa kuwa wana dhamira ya kufanya uovu dhidi ya Tanzania. “Natamani kila mmoja alibebe jambo hili kwa ukubwa, hawa watu hawatupendi, wanaangalia rasilimali zetu. Tukumbuke kuwa nchi yetu siyo masikini, kuna watu wanamezea mate rasilimali zetu. Ninawahakikishia kuwa tutailinda Tanzania na rasilimali zake kwa gharama yoyote ile, watameza mate hadi yataisha,” amesisitiza.

Amesema kuwa watumishi wa umma wanapaswa kubadilisha mtazamo kuhusu sekta, kuiheshimu na kuacha kuwaona walioko kwenye sekta hiyo ni watu wa chini. “Hatutaushinda umasikini kama tutaamini kwamba sekta binafsi ni maadui, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amebadilisha sheria inayomruhusu mkandarasi mzawa apate mradi mkubwa na wale wakubwa waombe sub-contract kwake, hili litatengeneza fursa za ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja viongozi wa Jukwaa la Wahariri.


No comments:

Post a Comment