
Na Beatus Maganja, Meatu
Wananchi wa Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu wanatarajiwa kuondokana na adha ya upatikanaji wa huduma za afya na elimu baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kwa kushirikiana na Kampuni ya Kitalii ya Mwiba Holdings Ltd. kuibua miradi ya ujenzi wa zahanati moja katika Kijiji cha Matale, madarasa manne na ofisi mbili za walimu katika Kijiji cha Mbughayabanyha.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia TAWA na wadau wake katika kutatua changamoto za wananchi na kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi zinanufaika moja kwa moja na rasilimali za wanyamapori.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika miradi hiyo Novemba 25, 2025 iliyofanyika katika vijiji hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Fauzia Ngatumbura aliipongeza TAWA Kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd. Kwa Kuibua miradi yenye tija na manufaa makubwa inayozingatia utu wa mtanzania na kutoa rai kwa wananchi kuthamini, kulinda na kutunza miradi hiyo.
"Niwapongeze sana TAWA Kwa kushirikiana na wadau wenu kwa usimamizi mzuri wa miradi hii na Kazi kubwa mliyoifanya, ambapo Kwa kushirikiana na wananchi mmeweza kuibua miradi kila Kijiji Kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika" alisema Mhe. Fauzia.
"Wito wangu kwenu wananchi ni kwamba muendelee kuuenzi uhifadhi, kutoa ushirikiano Kwa wahifadhi katika kulinda hifadhi zetu, kwasababu kupitia hifadhi hizi tunaweza kupata fedha za kigeni na fedha Kwa ajili ya miradi mingine mingi" aliongeza Mkuu huyo wa Wilaya ya Meatu.
Ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imefikia asilimia 63 unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya akina mama na watoto kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, huku madarasa na ofisi za walimu zilizofikia asilimia 75 zikitarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo inayotokana na shughuli za uhifadhi na utalii kupitia Uwekezaji Mahiri (SWICA) ndani ya hifadhi ya Maswa iliyoanza Oktoba 25, 2025 na kutarajiwa kukamilika Disemba 2025, Afisa Uhifadhi kutoka TAWA Kanda ya Ziwa Lusato Masinde alisema ujenzi wa zahanati ambayo itakuwa na wodi ya mama na mtoto, OPD na RCH itagharimu kiasi cha zaidi ya shillingi millioni 286 huku ujenzi wa madarasa manne na ofisi mbili za walimu ukigharimu kiasi cha shillingi millioni 216.7.
Baadhi ya wananchi wameeleza furaha yao kutokana na miradi hiyo, wakisema kuwa imefika wakati muafaka na itaongeza imani na matumaini kwa Serikali yao huku TAWA ikiahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kupitia miradi hii, Meatu inatarajiwa kupiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na TAWA.










No comments:
Post a Comment