Na Mwandishi Wetu
HALMASHAURI ya Mji Handeni imeainisha mikakati mitano ya kuimarisha utekelezaji wa afua za lishe, ili kukabiliana na changamoto za utapiamlo na kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na uzito pungufu.
Akisoma taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Lishe kwa Robo ya Kwanza, Novemba 11, 2025, Ofisa Lishe wa Halmashauri hiyo, Ester Herman, amesema mikakati hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu lishe bora na kuhakikisha huduma muhimu za lishe zinatolewa kikamilifu katika ngazi zote.
Ametaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni kuhamasisha jamii kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanaendelea kuhudhuria kliniki hata baada ya kukamilisha chanjo, na kushirikiana na idara za Elimu Msingi, Sekondari pamoja na Kamati za Lishe za Kata kuhamasisha wazazi kuchangia huduma za chakula shuleni.
Aidha, amesema Halmashauri imejipanga kuhimiza wajawazito kufika mapema kwenye vituo vya afya, ili kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na uzito pungufu, sambamba na kushirikiana na Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoa elimu ya kilimo na ufugaji bora wa kuku, bata na sungura ili kuongeza upatikanaji wa chakula chenye virutubisho.
Ester ameongeza kuwa Halmashauri pia itashirikiana na sekta mtambuka katika maadhimisho ya siku ya afya na lishe ngazi ya mtaa, kama njia ya kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika masuala ya lishe.
Hata hivyo, amebainisha kuwepo kwa changamoto kadhaa zinazohitaji ufuatiliaji wa karibu, ikiwemo baadhi ya wazazi kuchelewa kuwapeleka watoto wenye utapiamlo mkali vituoni kutokana na imani za kishirikina, na mahudhurio hafifu ya kliniki baada ya watoto kukamilisha ratiba ya chanjo.

No comments:
Post a Comment