KWAGILWA AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUHESHIMU NA KUZINGATIA MUDA WA KAZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 24, 2025

KWAGILWA AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUHESHIMU NA KUZINGATIA MUDA WA KAZI

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, amewataka watumishi wote walio chini ya Ofisi hiyo  kuripoti kazini saa 1:30 asubuhi na kutekeleza majukumu yao hadi saa 9:30 alasiri kama ilivyoanishwa katika Kanuni F.1 ya  Kanuni za Kudumu za Utumishi  wa Umma za mwaka 2009.


Mhe. Kwagilwa ametoa maelekezo hayo leo tarehe 24 Novemba, 2025 baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Kisasa jijini Dodoma majira ya saa 1:30 asubuhi na kubaini idadi kubwa ya walimu wa shule hiyo hawajaripoti  kazini kwa wakati ili kutekeleza wajibu wao kama ilivyokusudiwa na Serikali.


“Wakati nimefika hapa nimekagua kitabu cha maudhurio ya walimu na kubaini walimu 16 tu kati ya walimu zaidi ya 55 ndio waliowahi kazini, hivyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Mhe. Profesa Riziki Shemdoe ninaelekeza kuwa, watumishi wote walio chini ya OWM- TAMISEMI wakazingatie muda wa kufika kazini saa moja na nusu ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.” Amesisitiza Mhe. Kwagilwa.


Mhe. Kwagilwa amehimiza  kuwa dhamira ya maelekezo aliyoyatoa ni  lengo la msisitizo huo ni kuwakumbusha watumishi wa umma kufika kazini kwa wakati ili kuwahudumia wananchi, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora itakayopeleka  tabasamu kwa wananchi. 


Akizungumza kwa niaba ya walimu wa shule ya msingi Kisasa, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi. Jesca Mwarabu ameahidi kuwa yeye pamoja na walimu anaowaongoza watahakikisha wanazingatia muda wa kufika kazini ili waweze kutekeleza majikumu yao kikamilifu kwa mujibu wa sheria,kanuni,taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma.


Sanjari na hilo, Mhe. Kwagilwa amewataka Wakuu wa Wilaya kote nchini kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo hayo aliyoyatoa ili yawe na tija katika kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa walimu na watumishi wote umma walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI.


Aidha, Mhe. Kwagilwa amewaomba wazazi na walezi kuhakikisha wanawasajili watoto waliofikia umri wa kuanza shule za awali na msingi ili kupata muda wa maandalizi kwa ajili ya kuanza masomo mwaka 2026. 


Ziara hiyo ya Mhe. Reuben Kwagilwa, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu ililenga kujiridhisha na namna watumishi wa umma wanavyoheshimu muda wa kazi ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa umma.




No comments:

Post a Comment