
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, kwa kushirikiana na Wakala wa Vipimo (WMA), imeendesha mafunzo maalum kwa wauzaji wa gesi katika Mkoa wa Dodoma yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu usalama, uhalali wa biashara, na matumizi sahihi ya mizani katika upimaji wa gesi.
Mafunzo hayo yamefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na mawakala, wauzaji wa rejareja, wasambazaji, pamoja na wawakilishi wa halmashauri za jiji na wilaya.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma, Said Ibrahim, amesema lengo ni kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa mlaji zinakuwa na ujazo sahihi, hususan gesi ya kupikia ambayo matumizi yake yameongezeka kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
"Ni numuhimu kuhakikisha gesi wanayonunua na kuwauzia wateja iwe imepimwa kwa usahihi na njia pekee ya kufanya hivyo ni kutumia minzani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo,"amesema.
Aidha, amewakumbusha wafanyabiashara hao kwamba kutotumia vipimo sahihi ni kosa kisheria na kunaweza kusababisha hasara kwa mlaji na kwa mfanyabiashara mwenyewe.
Kwa upande wake afisa Vipimo kutoka WMA Mkoa Edward Patrick amehoji ni kwanini wafanyabiashara hao hawaweki mizani katika sehemu inayoonekana na wateja hawawapimii mitungi ya gesi kwasababu wengi wao wanakuwa nayo lakini wanaificha.
"Mbaya zaidi mkiikagua mara moja mmemaliza hamrudii tena kuikagua, unaweza ukakuta mtu mzani wa kuuzia sukari wenyewe wanaukagua kila mwaka lakini ule wa gesi kauweka ndani mpaka mteja aombe ndipo anautoa na umeshaaribika, mnatakiwa kuwa na mizani na muitumie,"amesema.
Naye Afisa udhibiti ubora kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA), Husna Kabaju amewataka wafanyabiashara wa mitungi ya gesi kuhakikisha wanakuwa na mikataba kutoka kwa mawakala wao.
Katika hatua nyingine baadhi ya wauzaji na wasambazi wa mitungi ya gesi wamesem mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwao kutikana elimu waliyoipata juu ya umuhimu wa kuwa na mizani ya kupimia mitungi ya gesi huku wakiomba yawe endelevu.
Mafunzo kama hayo yamekuwa yakitolewa na Wakala wa Vipimo mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kulinda haki ya mlaji na kuongeza uaminifu katika biashara ya bidhaa zinazohitaji vipimo sahihi, ikiwemo gesi ya kupikia.
Huku yakiweka msingi imara wa kuboresha biashara ya gesi katika mkoa wa Dodoma, ambapo inatarajiwa kuinua ubora wa huduma, kuongeza usalama, na kuimarisha taswira ya biashara ya LPG katika mkoa na taifa kwa ujumla.
Huku yakiweka msingi imara wa kuboresha biashara ya gesi katika mkoa wa Dodoma, ambapo inatarajiwa kuinua ubora wa huduma, kuongeza usalama, na kuimarisha taswira ya biashara ya LPG katika mkoa na taifa kwa ujumla.




No comments:
Post a Comment