
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Madini imeanza kujadili na kuweka Mikakati Kabambe ya kutekeleza maelekezo mbalimbali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa nyakati tofauti ikiwemo wakati akifungua Bunge la 13, hotuba yake ya kuwaapishwa Mawaziri, ahadi za siku 100 wakati wa Kampeni pamoja na ahadi za Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025-2030
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha rasilimali za madini zinaendelezwa na kusimamiwa kuongeza mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi, kuchangia katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwanufaisha wananchi moja kwa moja.
Akizungumza katika kikao kazi na Menejimenti ya Wizara kilichofanyika Novemba 24 na 25 2025, jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Rais Dkt. Samia ana matumaini makubwa na manufaa ya Sekta ya Madini ikiwemo kuona rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa halisi ya taifa na watanzania ikiwemo kuendesha uchumi wa nchi.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo ya Rais hauhitaji kusukumwa, bali unahitaji ari, kasi na ubunifu kutoka kwa Menejimenti ya Wizara na taasisi zake na kuongeza kwamba, Wizara inapaswa kuhakikisha maagizo yote yanayohusu mageuzi na uendelezaji wa sekta ya madini yanatekelezwa kwa ufanisi ili kuongeza mchango wake kwenye maendeleo ya nchi na katika Pato la Taifa.
Aidha, amemwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Madini kuwakutanisha wataalam wa Wizara na wazalishaji wa makaa ya mawe nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto zao, kupata maoni ya namna ya kuendeleza madini hayo yalete manufaa zaidi kwa taifa ikiwemo kukuza biashara na uzalishaji wa madini hayo.
‘’ Kuna viwanda vingi vya chuma na vingine nchi jirani ambavyo zinahitaji sana makaa ya mawe kuzalisha bidhaa mbalimbali, hii itawasaidia wazalishaji wetu kukuza biashara zao na Serikali kunufaika zaidi kupitia madini haya,’’ amesema Mhe. Mavunde.
Pia, Mavunde amesisitiza kuhusu dhamira ya Serikali kuanzisha kwa Mfuko wa dhamana (Export Guarantee Scheme) ambapo kupitia Mfuko huo wachimbaji watanzania wataweza kukopeshwa mitaji na Serikali na hivyo kufanya shughuli zao kwa tija zaidi badala ya kupata fedha hizo kutoka nje.
‘’ Wakisaidiwa hawa watawekeza nchini na tutapata manufaa zaidi kutokana na mnyororo wake lakini pia tunataka kuhamisha mfumo wa biashara ya dhahabu na vito utoke Dubai ufanyike hapa hapa nchini. Tunataka biashara hii ifanyike Geita, Chunya, Kahama, Arusha na kwingineko ili kuongeza manufaa zaidi ya sekta nchini na hatimaye Tanzania tutakuwa kitovu cha Madini, ’’ amesisitiza Mhe. Mavunde.
Pia, Waziri Mavunde ametaka maoni zaidi yatakayosaidia kuongeza makusanyo ya Serikali, kuimarisha usimamizi wa shughuli za madini, na kupanua fursa za kiuchumi kupitia sekta hiyo ikiwemo kuwaendeleza vijana na wanawake na kukuza ajira.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steve Kiruswa, amewataka watumishi wa Wizara kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na nidhamu ya hali ya juu. Amesema utekelezaji mahiri wa majukumu ndiyo msingi wa kuongeza maduhuli na kulinda rasilimali za taifa.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya madini nchini, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza ajira kwa watanzania, kukuza uchumi wa ndani na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa.
Awali, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, aliwasilisha maeneo 14 ya kipaumbele ambayo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyapa uzito katika hotuba na maelekezo yake mbalimbali kuhusu uendelezaji wa Sekta ya Madini.







No comments:
Post a Comment