Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa ruhusa kwa magari ya abiria kuanza kutumia barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya tatu inayoanzia katikati ya jiji la Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JNIA hadi Gongo la Mboto kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo ya Nyerere.
Ulega ametoa ruhusa hiyo leo Novemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo ambao umekamilika kujengwa kwa asilimia 100 na kusisitiza umuhimu wa barabara hiyo kuendelea kutumika hadi hapo mtoa huduma kwa ajili ya kuleta mabasi katika barabara hiyo atapopatikana.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kipindi hiki ambacho mabasi yaendayo haraka hayajawa tayari katika barabara hii ya Gongo la Mboto Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ipange utaratibu wa kuruhusu magari mengine yaweze kutumia barabara ili wananchi wapate nafasi ya kuendelea na shughuli zao na huduma kwa uharaka", amesisitiza Ulega.
Ulega amewaeleza wananchi wa Gongo la Mboto kuwa haiwezekani barabara zimejengwa na wananchi wenyewe na inakuwa vigumu kuitumia huku watu wakiendelea kukwama katika msongamano wa magari kila siku wakati wote.
Hapo awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alimuomba Waziri huyo aweze kuruhusu barabara za Mabasi yaendayo haraka zitumike na magari mengine yanayobeba abiria katika kipindi ambacho bado mabasi yaendayo haraka hayajaanza kutoa huduma.
Naye, Mfanyabiashara wa Chakula eneo la Gongo la Mboto, Bi Mariam John ameshukuru kwa miundombinu mbalimbali inayoendelea kujengwa hapa nchini na kutoa wito kwa watanzania kudumisha amani katika Taifa letu na kuomba lile lililotokea Oktoba 29, 2025 lisijirudie tena kwakuwa limegharimu maisha ya watu, uharibufu na upotevu wa mali na kusababisha watu kulala nyumbani wakati vipato vya wengine vinategemea mauzo ya kila siku.
"Niwaombe watanzania wenzangu kwa uchungu hatuhitaji yajirudie yaliyotokea mwanzo, tunahitaji amani, Amani ndio kila kitu katika nchi yetu, hii nchi imepambaniwa sana na Mwalimu Nyerere tuungane wote kujenga amani ndani ya nchi yetu", amesema
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS Eng. Malima Kusesa amesema barabara ya Mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu ina urefu wa kilometa 23.3 na imetekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 231.6 na Mkandarasi kampuni ya Sinohydro Corporation.
Ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Hali ya Usafiri katika Jiji la Dar es Salaam (DUTIP) pamoja na Serikali ya Tanzania.







No comments:
Post a Comment