Tarehe 27 Novemba 2025, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kimesheherekea Sherehe ya Mahafali ya 24. Ikiwa ni siku muhimu ya kuwapongeza wahitimu wa Ndaki hiyo kwa juhudi na uwajibikaji kitaaluma na kusherehekea mafanikio kwa wanafunzi na watumishi kwa ujumla.
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha alieleza juu ya maendeleo katika Ndaki ya Mbeya kuwa Ndaki hiyo imekuwa ikipiga hatua kila leo na hilo linadhihirishwa kwa idadi kubwa ya wahitimu na namna sherehe ya mahafali ilivyoratibiwa vema jambo ambalo linaendelea kukuza taswira ya Chuo Kikuu Mzumbe.
Aliongeza kuwaasa wahitimu wote kuhusu kuwa mabalozi wema wa Mzumbe na kutumia maarifa na ujuzi walioupata Chuoni kwa kuleta tija katika jamii zinazowazunguka. Pia, alitoa rai kwa mashirika na taasisi zilizohudhuria mahafali hayo kuwatumia wahitimu wa Mzumbe kwani wamepikwa vema na wenye uwezo wa kuwasilisha matokeo chanya kazini.
Baada ya wahitimu kutunukiwa Shahada rasmi na Mkuu wa Chuo, Dkt. Ali Mohamed Shein, Mkuu wa Chuo aliwapongeza na kuwasisitiza juu ya uadilifu na uchapakazi kwa ajili ya maendeleo binafsi na ya jamii yote kama ilivyo kauli mbiu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Tujifunze Kwa Maendeleo ya Watu.
Aidha, Bw. William Kibona, Mwanafunzi bora wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya mwenye GPA ya 4.7 Shahada ya Uhasibu na Fedha, alieleza kuwa ili kufanikiwa yapaswa kumtanguliza Mungu kwanza na kuwa na nidhamu katika kutimiza malengo. Pia, aliushukuru uongozi wa Ndaki ya Mbeya chini ya Rasi wa Ndaki hiyo, Prof. Henry Mollel kwa malezi mazuri ya kitaaluma na uendeshaji yaliyochangia mafanikio yake na wahitimu wote.
Wazazi, walezi wa wahitimu na wageni waalikwa wamesifia Sherehe ya Mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, kwa kuongeza idadi ya wahitibu bora jambo linalodhihirisha kuwa Chuo Kikuu Mzumbe ni chuo bora zaidi.





No comments:
Post a Comment