MIRADI IKAMILIKE KWA MANUFAA YA WANANCHI - PROF. SHEMDOE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 26, 2025

MIRADI IKAMILIKE KWA MANUFAA YA WANANCHI - PROF. SHEMDOE




Na James K. Mwanamyoto, OWM TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka watendaji walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI na taasisi zake, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ukamilishaji wa miradi ya maendeleo iliyopo katika hatua ya utekelezaji ili ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo, wakati wa kikao kazi chake maalum na Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Idara na Vitendo vya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI pamoja na Taasisi zote zilizopo chini ya ofisi hiyo.

“Ni vema mkaona namna bora ya kukamilisha miradi inayotekelezwa ili iwanufaishe wananchi, hivyo hakikisheni miradi yote iliyoanzishwa inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi,” Prof. Shemdoe amesisitiza.

Aidha, Prof. Shemdoe ameelekeza kuangaliwa upya suala la ujenzi wa masoko ya ghorofa kwenye Halmashauri kama yanakidhi uhitaji, kwani uzoefu unaonesha kuwa wananchi hususani wajasiriamali hawapendi kufanya shughuli zao ghorofani.

“Mfano mzuri ni soko la Machinga Complex Dar es Salaam, ambapo wananchi wengi wanapanga bidhaa zao barabarani badala ya kutumia vizimba vilivyo ghorofani, hivyo tutathmini kama kuna haja ya kujenga masoko ya ghorofa?” ametoa angalizo Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameshauri kuwa, iwapo itaafaa yajengwe masoko kama lililivyo la Machanga Complex Dodoma ambalo linawawezesha wafanyabiasha na wajasiriamali kujipatia kipato kwa kupanga bidhaa zao kwenye meza au vizimba walivyoandaliwa sokoni, na kuongeza kuwa hata gharama ya ujenzi wake ni ndogo ukilinganisha na ujenzi wa masoko la ghorofa.

Prof. Shemdoe amefanya kikao kazi hicho maalum na Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, ambapo ametumia kikao kazi hicho kuhimiza uwajibikaji utakaoiwezesha ofisi anayoisimamia kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora zitakazopelekea wananchi hususani wa kipato cha chini kupata tabasamu ndani ya nchi yao.

No comments:

Post a Comment