Tanzania, Korea zapanda mbegu ya ushirikiano mpya wa kiuchumi - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 26, 2025

Tanzania, Korea zapanda mbegu ya ushirikiano mpya wa kiuchumi


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kupitia Jukwaa la Biashara la Tanzania–Korea (Tanzania–Korea Business Forum) lililowakutanisha wadau wa uwekezaji na biashara wa serikali na sekta binafsi kutoka mataifa yote mawili.

Akifungua jukwaa hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amesema Tanzania na Korea zinaunganishwa na dira ya pamoja ya ustawi, ubunifu na maendeleo ambayo ndio msingi wa kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa hayo.

Mhe. Kombo ameongeza kuwa licha ya kukua kwa biashara kati ya Tanzania na Korea, bado upo uwanda mkubwa wa kuongeza ushirikiano huo haswa katika eneo la bidhaa za chakula, viwanda vya vifungashio na usindikaji wa bidhaa.

Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Mhe. Eun Ju Ahn, ameelezea furaha yake, kuona kampuni za Korea zikiwekeza Afrika na kuahidi ushirikiano wa karibu katika kubadilishana taarifa muhimu zitakazorahisisha kuimarisha ushirikiano huo wa uwili.

Balozi Ahn aliendelea kueleza kuwa miongoini mwa sababu zinazoifanya Tanzania kuendelea kuwa kituo bora cha uwekezaji, ni pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya vijana inayowahakikishia wawekezaji uwepo wa rasilimali watu na soko la bidhaa na huduma wanazozalisha.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dkt. Latifa M. Khamis, amebainisha ongezeko la mauzo ya Tanzania kwenda Korea kutoka dola za kimarekani milioni 22 hadi 28 mwaka 2024, yakichochewa na bidhaa za kilimo na madini. Aidha, Dkt. Khamis amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Korea kushiriki katika maonesho ya Sabasaba Tanzania.

Jukwaa hilo limehitimishwa kwa kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kistratejia kati ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Chama cha Waagiza Bidhaa za Nje Korea (KOIMA)








No comments:

Post a Comment