NDEJEMBI: TANZANIA SASA INA UMEME WA KUTOSHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 26, 2025

NDEJEMBI: TANZANIA SASA INA UMEME WA KUTOSHA



Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Tanzania kwa sasa ina umeme wa kutosha na hivyo ukamilifu wa Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere umeondoa kabisa mgao wa umeme nchini.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo leo Novemba 26, 2025 wakati wa ziara yake katika Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) iliyoleng kujionea namna mradi huo unavyozalisha umeme na kujihakikishia kuwa uzalishaji unaendelea kwa ufanisi kama ilivyopangwa.

Waziri Ndejembi amesema kuwa tayari mradi wa Julius Nyerere umekamilika na una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, kiwango ambacho kimeleta uthabiti wa upatikanaji wa nishati na kupunguza changamoto za upatikanaji umeme zilizokuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo nchini.

"Tangu uzalishaji ulipoanza hapa, kumekuwa na maboresho makubwa katika usambazaji wa umeme na sasa Serikali inajikita kwenye ujenzi wa njia za kusambaza umeme ili kuufikisha katika maeneo mengi zaidi nchini”. Amesisitiza Mhe. Ndejembi

Amefafanua kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha mradi umekamilika kwa wakati na una uwezo wa kutoa umeme katika eneo la mradi na kuwafikia Watanzania.

Kuhusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa ujenzi unaendelea, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuhakikisha umeme wa uhakika unafika katika mikoa ya Kati, Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Aidha, amesema Serikali ipo katika hatua za kuanza ujenzi wa njia nyingine muhimu ya kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi wa JNHPP hadi Mkuranga, ambayo itapeleka umeme katika Kongani ya Viwanda Mkuranga ambao pia utalisha Jiji la Dar es Salaam.

"Uhai wa mradi huu unategemea sana utunzaji wa rasilimali maji, asilimia 80 ya maji ya bwawa yanatoka Mto Kilombero na asilimia 20 kutoka Mto Ruaha na mito mingine midogo. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maji, Maliasili na Utalii, Mifugo pamoja na TFS kulinda vyanzo hivyo," amesema Ndejembi

Ameeleza kuwa endapo vyanzo vya maji vitatunzwa ipasavyo, Tanzania ina uwezo wa kupata umeme wa uhakika kwa zaidi ya miaka 100 kupitia chanzo hicho cha Julius Nyerere.

Ndejembi amewataka Watanzania kutambua kuwa mradi huo ni kwa faida yao wenyewe, hivyo ni muhimu kuulinda na kuuthamini.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema kuwa uwekezaji unaoendelea wa Tanesco katika miradi ya umeme umefikia Shilingi trilioni 13.5.


Bw. Twange amebainisha kuwa, kati ya miradi 41 inayoendelea, miradi sita ni ya kuzalisha umeme na 35 ni ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme.


"Kwa sasa Tanzania ina umeme wa ziada na hakuna mgao, isipokuwa yanapotolewa matangazo ya kuzimwa kwa baadhi ya maeneo kwa muda mfupi ni wa ajili ya maboresho mbalimbali ya miundombinu," amesema Twange.


Ameongeza kuwa, TANESCO inaendelea kuboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya viwanda, ikiwemo ujenzi wa njia ya umeme kutoka Mkuranga kuelekea Chalinze, Kibaha na Kwala, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 3 zimewekezwa ili kuhakikisha viwanda vinapata nishati iliyo ya uhakika.


Vilevile amesema kuwa miradi mipya ya umeme wa jua na umeme wa maji inaendelea, ikiwemo mradi wa Kishapu Shinyanga wa Megawati 50 na Malagarasi Kigoma wa Megawati 49.5, ambayo itaunganishwa kwenye gridi ya Taifa muda si mrefu.


Akizungumzia agizo la Rais la kuanza maandalizi ya kuzalisha umeme wa nyuklia, Bw. Twange ameema tayari mazungumzo yanafanyika na wawekezaji mbalimbali, na Wizara ya Nishati iko kwenye hatua za mwisho za maandiko ya awali kabla ya vikao vya wadau kuanza.


Bw. Twange amesisitiza kuwa Tanzania ina umeme wa kutosha na mwekezaji yeyote anayehitaji nishati kwa ajili ya viwanda au shughuli nyingine anakaribishwa kuja nchini, kwani Tanesco iko tayari kumhudumia bila changamoto ya upungufu wa umeme.


Ziara hiyo ni mwendelezo wa Ziara za Waziri wa Nishati kuzitembelea taasisi zilizo chini yake kwa lengo la kutambua namna shughuli za Taasisi hizo zinavyoendeshwa.



No comments:

Post a Comment