MNADA WA MADINI YA VITO WAONGEZA UWAZI NA KUDHIBITI UTOROSHAJI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 27, 2025

MNADA WA MADINI YA VITO WAONGEZA UWAZI NA KUDHIBITI UTOROSHAJI NCHINI

Arusha, Novemba 27, 2025

Sekta ya madini inaendelea kunufaika na mageuzi ya kidijitali, baada ya mfumo wa mnada wa madini ya vito kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kuonyesha matokeo chanya katika kuongeza uwazi, ushindani na kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.

Akizungumza katika mnada wa tatu wa madini ya vito uliofanyika katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, CPA Venance Kasiki, amesema mfumo huo umeleta mapinduzi katika namna wafanyabiashara wanavyonunua madini.

Kasiki amesema kupitia TMX, ununuzi unafanyika kwa njia ya kidijitali na kwa uwazi mkubwa ambapo washiriki wote wanaona hatua kwa hatua mwenendo wa bei, hatua inayotofautiana na utaratibu wa zamani wa matumizi ya bahasha ambao haukuwa na uwazi wa kutosha.

Ameeleza kuwa mageuzi hayo yameongeza hamasa kwa wafanyabiashara kushiriki kwa wingi katika minada, huku Serikali ikipata mapato halali na wauzaji wakipata bei stahiki. “Mfumo huu unaimarisha uwazi na ushindani, na hatimaye kuongeza mapato ya serikali. amesisitiza Kasiki.

Kasiki ameongeza kuwa hatua hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoroshaji wa madini, kwani mfumo wa soko umeweka uwazi wa bei na malipo, huku Tume ya Madini ikiendelea kuimarisha mazingira ya biashara kupitia uanzishwaji wa masoko 44 na vituo 117 vya ununuzi wa madini nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Biashara kutoka TMX, Nicolaus Kaserwa, amesema mfumo wa kidijitali unahakikisha bei inashindanishwa kwa uwazi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mnada, hivyo kujenga imani kwa wadau wote wa sekta.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Soko la Madini mkoa wa Arusha, Akwiline Lissu, amewataka wafanyabiashara kuendelea kutumia mfumo huo akisema unarahisisha upatikanaji wa madini bila ulazima wa kufuatilia kwa mtu mmoja mmoja au kusafiri umbali mrefu.

Ameshukuru Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuendeleza mageuzi yanayofanya biashara ya madini ya vito kuwa ya kisasa, salama na yenye tija kwa taifa.

No comments:

Post a Comment