Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amekosoa vikali taarifa zilizochapishwa na chombo cha habari cha kimataifa cha CNN kuhusu matukio ya tarehe 29 Oktoba, 2025, na kusema kuwa ripoti hiyo ina upungufu mkubwa wa kimaadili na weledi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere, Msigwa alieleza kuwa Serikali haikubaliani na jinsi CNN ilivyoshindwa kutoa taswira ya kiuhalisia kuhusu matukio hayo kwa upande wa Tanzania.
“Uhakiki wa maudhui yaliyomo katika makala ile unaendelea, lakini ni dhahiri kwamba CNN imeendelea kufanya makosa ya kiweledi na kiuadilifu. Kawaida, chombo cha habari cha kimataifa kama CNN kinapaswa kuzingatia weledi na maadili katika uandishi wake, lakini cha kushangaza ni jinsi walivyoshindwa kutafuta na kutunga ripoti yenye upande wa pili wa mada. Hii inadhihirisha makosa ya kitaaluma na kimaadili,” alisema Msigwa.
Akiendelea kutoa maelezo kuhusu makosa yaliyomo katika ripoti hiyo, Msigwa alisisitiza kuwa siyo kweli kwamba CNN ilishindwa kuwasiliana na Serikali au mamlaka zinazohusika kabla ya kuandika habari hiyo.
“Serikali inatoa wito kwa CNN na vyombo vya habari vingine vya kimataifa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari kwa kuwasiliana na mamlaka husika ili kutoa taarifa zilizothibitishwa, za kweli, na zisizo na mapendeleo,” aliongeza.
Msemaji huyo alisema kwamba picha zilizotumika na CNN kwenye ripoti hiyo, ambazo zilipigwa kwa simu wakati wa vurugu, hazikutoa picha kamili ya kile kilichokuwa kikiendelea.
Msigwa alieleza kuwa taarifa zinazochapishwa bila kuzingatia vyanzo rasmi zinahatarisha usalama na utulivu wa jamii na zinapotosha ukweli. Alionya kuwa ni muhimu kwa vyombo vya habari kutoa taarifa za pande zote ili kuweka wazi ukweli wa kila jambo.
“Serikali inahitaji uandishi wa habari unaojali pande zote na unatoa nafasi ya kutosha kwa kila upande kuelezea mtazamo wake. Si busara kuchagua upande mmoja wa habari bila kutoa nafasi kwa wengine,” alisema Msemaji Msigwa.
Kufuatia makala hiyo ya CNN, Msigwa alisisitiza kwamba Serikali itendelea kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa vyombo vya habari, hasa wakati ambapo taarifa zinazohusu nchi zinapochapishwa na vyombo vya kimataifa. Alisema kwamba Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya vyombo vya habari ambavyo vitashindwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.
Aidha, Msigwa alifafanua kuwa Serikali itakuwa na mashauriano na CNN na vyombo vingine vya habari vya kimataifa ili kuhakikisha kwamba habari zinazoandikwa kuhusu Tanzania zinakidhi viwango vya kimaadili na weledi.
Alikaribisha vyombo vya habari vya kimataifa kuja Tanzania na kuzungumza na Serikali pamoja na wananchi ili kupata taarifa sahihi na za kina.
“Tunasisitiza kuwa vyombo vya habari vya kimataifa, kama CNN, vinapaswa kuandika habari kwa njia inayozingatia ukweli na usawa. Tunawaomba waache kuchagua kuripoti upande mmoja na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa zisizo na vyanzo halali na rasmi,” alimaliza kusema Msemaji Mkuu wa Serikali.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari vya ndani na nje kutoa taarifa kwa usahihi, bila kupotosha, na kwa kuzingatia pande zote za suala linalozungumziwa.


No comments:
Post a Comment