
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi waliohusika na uzembe wa kutoshughulikia tatizo la mizani ya Mikese mkoani Morogoro, jambo lililosababisha foleni na usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Ulega ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya dharura (CERC) mkoani Morogoro ambapo akiwa njiani alishuhudia msongamano mkubwa wa magari na alipofuatilia ndipo aliambiwa chanzo ni kuharibika kwa mzani.
“Hili jambo la foleni hapa Mikese limezoeleka, watu wanateseka na tunaharibu biashara za watu na uchumi wa nchi yetu kwa sababu foleni ina msongamano huu ni mkubwa kiasi cha kufika katika kijiji cha jirani. Hii haiwezi kukubalika. Wananchi wanateseka kwa kukaa njiani muda mrefu. Biashara zinadumaa. Sitaki kumuonea mtu nataka majibu nani amesababisha hili na kuchukua hatua kwa haraka, amesema Ulega.

Akiwa hapohapo Mikese, Ulega alipiga simu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aisha Amour, na kumtaka asimamishe wahusika wote wa mzani huo ili kuchunguza tatizo linatokana na nini ili wale watakaobainika kuhusika na uzembe huo, wachukuliwe hatua.
“Katibu Mkuu nakuagiza, wasimamishe watumishi wote walio kwenye mamlaka yangu mpaka nipate kujua chanzo na sababu ya tatizo hili na nani anayefanya uzembe wa jambo hili”, amesisitiza Ulega.
Katika hatua nyingine, Ulega amemwagiza Mhandisi Aisha kuhakikisha timu ya wataalamu inafika Mikese na kutengeneza mzani huo ili kero hiyo imalizike na mateso kwa watumiaji wa njia hiyo yapungue.
Mizani ya Mikese mkoani Morogoro ni miongoni mwa maeneo maarufu nchini kutokana na wingi wa magari yanayopita kwa siku kuelekea katika mikoa tofauti nchini na mengine nje ya nchi.







No comments:
Post a Comment