Na Carlos Claudio, Dodoma.
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetoa taarifa muhimu kwa umma kuhusu majumuisho ya zoezi la udahili wa wanafunzi wa Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2025/2026, likiambatana na maelekezo mahsusi kwa vyuo na wanafunzi wote nchini.
Akizungumza leo Novemba 17, 2025 jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, amesema maombi ya programu za afya na sayansi shirikishi kwa Tanzania Bara yalifanyika kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (CAS), huku Zanzibar maombi yakifanyika moja kwa moja vyuoni.
Kwa upande wa kozi zisizo za afya, maombi yalitumwa moja kwa moja vyuoni na kisha majina ya waliochaguliwa kuwasilishwa kwa NACTVET kwa ajili ya uhakiki.
Dkt. Lingwanda amesema jumla ya waombaji 49,148 waliwasilisha maombi ya kujiunga na vyuo mbalimbali, ambapo 39,553 sawa na asilimia 80% walichaguliwa. Kati yao, wanawake ni 20,131 (51%) na wanaume 19,422 (49%).
“Kwa upande wa kozi zisizo za afya, jumla ya wanafunzi 108,109 waliochaguliwa na vyuo waliwasilishwa kwa NACTVET kwa uhakiki, na kati yao 106,022 (asilimia 98%) walithibitishwa kuwa na sifa stahiki za kujiunga na programu walizoomba,” amesema Dkt. Ligwanda
Aidha Dkt. Lingwanda ameibua changamoto kadhaa zilizojitokeza wakati wa udahili, ikiwemo baadhi ya vyuo kuchagua waombaji wasio na sifa stahik, vyuo kuwasilisha maombi ya udahili kwa niaba ya waombaji bila ridhaa yao pamoja na Kutumia namba za simu ambazo si za waombaji.
Amesema asilimia 2% ya waombaji walichaguliwa kwenye kozi ambazo hawana sifa, jambo lililothibitika wakati wa uhakiki.
NACTVET imetoa fursa maalum kwa wanafunzi walioathirika kufanya marekebisho ya programu ili kuomba kozi wanazokidhi sifa. Fursa hii itakuwa wazi hadi Novemba 30, 2025.
Ameongeza na kusema kuwa elimu imetolewa kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa utoaji sahihi wa taarifa zao huku akisema serikali kupitia Wizara ya Elimu imetangaza kufunguliwa kwa vyuo kwa awamu mbili: Wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuanzia Novemba 17 na Wanafunzi wanaoendelea na masomo kuanzia Novemba 24, 2025
Vyuo vimetakiwa kuwasajili wanafunzi wote waliochaguliwa na kufika chuoni ndani ya muda rasmi (17 Novemba – 12 Desemba 2025). huku vikikatazwa kupokea wanafunzi ambao hawajachaguliwa rasmi.
Wanafunzi wametakiwa Kuripoti katika vyuo walivyochaguliwa na kujisajili kwa wakati na baada ya kusajiliwa chuoni, kuingia kwenye tovuti ya NACTVET (www.nactvet.go.tz) na kuhakiki taarifa zao kupitia sehemu ya “student’s information verification” na Kuripoti kasoro zozote kwa chuo au NACTVET mara moja.
Dkt. Lingwanda amesisitiza kuwa mwanafunzi asiposajiliwa kwenye mfumo, atakosa Award Verification Number (AVN)na anaweza kukumbana na matatizo makubwa ya uthibitisho wa vyeti baada ya kuhitimu.
Hali hii husababisha wanafunzi kukwama wakati wa usajili hivyo NACTVET imetangaza kuwepo kwa dawati maalum kusaidia wanafunzi na vyuo katika kipindi chote cha usajili.
MAWASILIANO:
Namba ya bure: 0800 110 388
WhatsApp: 0736 310 311
Barua pepe: info@nactvet.go.tz
Mitandao ya kijamii: Facebook, Twitter, Instagram
Baraza limehitimisha kwa kuwataka wanafunzi na vyuo kufuata taratibu na miongozo, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka utaratibu.






No comments:
Post a Comment