NAIBU WAZIRI QWARAY ASISITIZA UWAJIBIKAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 27, 2025

NAIBU WAZIRI QWARAY ASISITIZA UWAJIBIKAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, ametoa wito kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria kote nchini kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya Sheria, Kanuni na Maadili ya Utumishi wa Umma.

Ameyasema hayo leo Novemba 27, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, wakati akifungua kikao kazi cha watendaji hao kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Qwaray alisisitiza kuwa serikali haitavumilia uzembe, uvunjaji wa taratibu, wala ucheleweshaji wa haki kwa watumishi.

“Ninasisitiza — hatutaendelea kupoteza fedha za serikali kutokana na makosa madogo madogo yanayotokana na kutowajibika kwenu. Ni lazima tubadilike,” alisema Mhe. Qwaray akizungumza kwa msisitizo mbele ya washiriki wa kikao kazi hicho.


Ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la mashauri ya nidhamu yanayoishia kuipa Serikali hasara kupitia rufaa zinazoshindwa kutokana na kushindwa kufuata taratibu sahihi za kisheria.

“Makosa ya kuandika vibaya hati za mashtaka, kutowahoji mashahidi au kumpa mtumishi haki ya kujitetea yamesababisha serikali kulipa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwenye maendeleo,” ameongeza.

Naibu Waziri Qwaray amewataka watendaji hao kusoma na kuelewa kikamilifu Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298, Kanuni za Utumishi wa Umma za 2022, pamoja na nyaraka nyingine muhimu ili kuondoa mwanya wa kufanya makosa ya kiutumishi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa watumishi kuwa wazalendo hususan katika kipindi cha baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, akiwataka kuendelea kulinda amani, kutoa huduma bila upendeleo na kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta mgawanyiko katika jamii.


“Watumishi wa Umma ni kioo cha Serikali. Ni lazima muonyeshe uadilifu, mtangulize maslahi ya Taifa, na kuwa mfano wa kutegemewa na wananchi,” amesema Qwaray.

Pia amewakumbusha Maafisa Utumishi kuwa na nyaraka za msingi mezani kila wakati, ikiwemo Katiba, Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, na Mpango Mkakati wa Taasisi kama nyenzo za kupanga na kusimamia utendaji wa kazi.

Naibu Waziri Qwaray amewahimiza washiriki kutumia kikao kazi hicho kutoa maoni kwa uwazi, kujadiliana kwa kina na kuibua suluhisho la changamoto zinazowakabili ili kuboresha utoaji huduma kwa umma. “Mnapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko tunayoyahitaji. Serikali inategemea uhodari wenu,” alisisitiza kabla ya kutamka rasmi kikao hicho kuwa kimefunguliwa.

No comments:

Post a Comment