
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wimbi jipya la vijana nchini limeanza kujitokeza kwa uthubutu kuwania nafasi za juu za uongozi wa kitaifa, likilenga kuonesha uwezo na mchango wa kizazi kipya katika kujenga taifa lenye usawa na uwajibikaji.
Miongoni mwa vijana hao ni Mwalimu Peter Frank, anayejulikana zaidi kama Mr. Black, ambaye ametangaza rasmi kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiwa na umri wa miaka 35 pekee, Mr.Black anatajwa kuwa miongoni mwa wagombea wachache vijana wanaothubutu kuvunja ukuta wa kizamani katika siasa za Tanzania.
Akizungumza jijini Dodoma, Mr. Black alisema hatua yake inalenga kuhamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uongozi wa taifa, hususan kwenye Bunge la Tanzania, ambako maamuzi muhimu ya kitaifa hufanyika.
“Tunapaswa kuamini kwamba vijana wana uwezo wa kusimamia kanuni, taratibu na misingi ya haki katika Bunge letu. Tunahitaji chombo kinacholeta usawa kwa kila mbunge na chenye kutoa dira ya maendeleo kwa wote,” amesema.
Kwa mujibu wa Mr. Black, malengo yake makuu ni kusimamia nidhamu na haki ndani ya Bunge, pamoja na kuongeza tija na nguvu za vijana katika kuendesha shughuli za maendeleo ya taifa.
Anasema vijana ni nguzo muhimu ya maendeleo, hivyo wanapaswa kupewa nafasi pana zaidi katika uongozi ili kutumia ubunifu na mawazo mapya kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

No comments:
Post a Comment