SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WANANCHI UMEME WA UHAKIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 25, 2025

SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WANANCHI UMEME WA UHAKIKA



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema, Serikali inawahakikishia wananchi upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwataka wananchi wa Dodoma na wadau mbalimbali kuwekeza katika shughuli za kiuchumi zinazohitaji umeme bila ya shaka yoyote kwani umeme upo wa kutosha na wa uhakika.

Naibu Waziri Salome Makamba ameyasema hayo leo tarehe 25 Novemba, 2025 mara baada ya kutembelea Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza umeme cha Zuzu kilichopo Jijini Dodoma na kueleza kuridhishwa kwake na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa mafanikio makubwa katika Kituo hicho.

Ameeleza kuwa wakati kituo hicho kinaanzishwa mwaka 1986 mahitaji ya umeme katika Kituo hicho yalikuwa MW 2 .5 tu lakini kwa sasa mahitaji ya umeme kwa Mkoa wa Dodoma ni MW 86.

“Serikali ya awamu ya sita inaendelea kukijengea uwezo kituo hiki inajenga njia ya umeme kutoka Chalinze kuja Dodoma- Zuzu wenye uwezo wa kilovoti 400 ikikamilika inauwezo wa kusafirisha umeme unaozalishwa Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere (Megawati 2,115),” amesema Mhe. Makamba

Sambamba na hayo, amewasihi waliopewa dhamana ya kusimamia Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Zuzu kukisimamia vema na kuhakikishwa kinalindwa dhidi ya uharibifu wa Mitambo mikubwa iliyonunuliwa kwa gharama kubwa.

“Mafundi mitambo waaendelee kufanya matengenezo yanayohitajika kwa wakati ili kuitunza mitambo hiyo muhimu ya kupoza na kuzalisha umeme,” amesisitiza Mhe. Makamba

Katika hatua nyingine , Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji Umeme Mha. Athanasius Nangali, amempongeza Naibu Waziri Salome Makamba kwa kuchaguliwa kuwaongoza katika Sekta hii muhimu ya Nishati na amemuahidi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa kuhusu ulinzi wa miundombinu ya umeme na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.

"Kwa niaba ya Watumishi wa TANESCO, tutaendelea kufanya kazi kwa weledi na kuwahudumia wateja vizuri," amesema Mha. Nangali.



No comments:

Post a Comment