
Na Witness Masalu WMJJWM-Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameelekeza watumishi wa Wizara hiyo kutekeleza na kuishi kauli mbiu ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele” kupitia utoaji wa huduma kwa kasi zaidi, karibu zaidi na wananchi.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Wizara hiyo kilichofanyika Novemba 25, 2025 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amewataka watumishi hao kujipambanua na kufanya kazi maradufu ya walichokua wanakifanya awali ili kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma kwa makundi yote katika jamii kwa ubunifu na ubora zaidi.
“Mnazo funguo za kuwezesha mabadiliko ya fikra za jamii ili waweze kuona mawanda mapana ya fursa za maendeleo na ustawi hivyo, inahitajika kasi na ukaribu zaidi na wananchi ili kufanikisha matamanio ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuleta tabasamu kwa jamii. Endapo mtumishi hatoendana na kasi hii itabidi tumtafakari jinsi ya kumsaidia” amesema Dkt. Gwajima.
Vilevile Dkt. Gwajima amewataka watumishi kupunguza mlolongo mrefu wa kutoa huduma kwa wananchi ili kuweka mazingira chanya ya kuwakimbilia na kuwatatulia changamoto zao kwa uharaka.
“Natarajia Taasisi zetu zitaimarisha mawasiliano na wananchi ili waweze kutukimbilia na kuondoa kero ambazo hazina ulazima na kuwapata matumaini mapya yenye tabasamu chanya “ amesema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Maryprisca Mahundi amewaagiza watumishi kuhakikisha wanaongeza tabasamu la wananchi kwa kuongeza ufanisi na ubora wa huduma wanazozitoa.
“Twendeni tukafanye kazi kwa umoja wetu bila kubaguana na kutumia karama tulizopewa na Mwenyezi Mungu ili tutimize maono ya Mhe.Rais ambayo ni kuleta maendeleo na Ustawi katika Jamii" amesema MaryPrisca.

Aidha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu amesema Wizara iko tayari kutekeleza yale yote yaliyoelekezwa na Mhe. Waziri kwa manufaa ya Taifa na Jamii kwa ujumla.


No comments:
Post a Comment