TENGENI MUDA KUWASIKILIZA WATUMISHI NA WANANCHI KWA LUGHA YA STAHA - PROF. SHEMDOE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 25, 2025

TENGENI MUDA KUWASIKILIZA WATUMISHI NA WANANCHI KWA LUGHA YA STAHA - PROF. SHEMDOE




Na James K. Mwanamyoto, OWM TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, viongozi katika Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga muda wa kusikiliza kero na malalamiko ya watumishi wa umma pamoja na wananchi kwa lugha ya staha.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi uliohudhuriwa na Wenyeviti wa Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, unafanyika katika Ukumbi wa Sephile Sapphire Pride uliopo jijini Dodoma.

“Tuwasikilize watumishi wenzetu pamoja na wananchi kwa lugha ya staha, tutachukua hatua ya kumuondoa yeyote atakayeshindwa kuwasikiliza watumishi na wananchi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, suala hili la kuwasikiliza watumishi na wananchi lizingatiwe na Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo katika Halmashauri zote nchini ili waweze kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Prof. Shemdoe amehimiza kuwa, moja ya jukumu la viongozi walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI ni kuwatumikia watanzania hivyo kila aliyebahatika kupata nafasi ya uongozi ahakikishe anawatumikia watanzania kwa ufanisi na uzalendo.

“Sisi watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI tunao wajibu wa kipekee wa kuleta tabasamu kwa wananchi, tukitimiza kikamilifu jukumu la kutoa huduma bora,” amesema Prof. Shemdoe.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Bw. Atupele Mwambene amesema, Walimu Wakuu walioudhuria mkutano huo ndio wenye jukumu la kupeleka tabasamu kupitia malezi watakayoyatoa kwa walimu wanaowasimamia na hatimaye wanafunzi watapata uelewa na ufaulu mzuri.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Bw. Didas Bambaza amemuahidi Prof. Shemdoe kuwa, Walimu Wakuu watakwenda kutekeleza kwa vitendo maelekezo yote aliyoyatoa ili huduma zitakazotolewa katika shule zote zilete tabasamu kwa wanafunzi na wananchi.

Kaulimbiu ya Mkutano Mkuu huo wa Saba wa Mwaka wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (TAPSHA) ni Mtaala Ulioboreshwa kwa Elimu Bora; Ujuzi na Ubunifu kwa Maendeleo endelevu ya Taifa.



No comments:

Post a Comment