
Na Meleka Kulwa, OKULY BLOG – Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi baada ya kupeleka timu ya wataalamu katika Viwanja vya Mnadani Msalato jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto.
Hatua hiyo inalenga kuwafikia wananchi ambao mara nyingi hukosa muda au fursa ya kufika hospitalini kupata huduma muhimu za afya.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BMH, Teophory Mbilinyi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Abel Makubi, ametoa wito kwa wananchi wa Msalato na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kupata matibabu na ushauri wa kibingwa.
“Huduma hizi ni za kwenu. Tunawaomba wananchi mjitokeze ili kwa pamoja tujenge taifa lenye afya bora,” amesema Mbilinyi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wauguzi wa BMH, Bi. Mwanaidi Makao, amewahimiza wakazi wa Msalato kutumia kikamilifu huduma zinazotolewa, huku akibainisha kuwa BMH itaendelea kurudi kwa awamu tofauti kutoa elimu na huduma za afya katika maeneo yenye uhitaji.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Ubunifu ambaye pia ni Mratibu wa Masuala ya Ukatili wa Kijinsia, Bi. Hindu Ibrahim, amesema timu hiyo haikufika Msalato kwa ajili ya kutoa elimu pekee bali pia kuhudumia wananchi moja kwa moja kupitia vipimo mbalimbali, uchangiaji damu na huduma za afya ya akili.
“Tunafahamu Msalato ni eneo linalokusanya watu wengi mwisho wa wiki, wengine hukosa muda wa kwenda hospitali. Ndiyo maana tumewafuata,” ameeleza Bi. Hindu.
Baadhi ya wananchi waliohudumiwa wamesema huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa kwao.
Ratifa Abdalah, mkazi wa Miyuji, amesema uchangiaji damu ni jukumu la Watanzania wote ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu hospitalini.
Naye Sauda Omary, mkazi wa Msalato, ameishukuru BMH kwa kusogeza huduma karibu na jamii, akisisitiza umuhimu wa wananchi kupima afya mara kwa mara ili kujua hali zao.
Huduma hizo ni mwendelezo wa jitihada za BMH kuimarisha afya za wananchi na kuunga mkono kampeni za kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini.










No comments:
Post a Comment