RC MTAKA ATOA WITO KWA VIJANA NA WANANCHI NJOMBE KULINDA AMANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, December 7, 2025

RC MTAKA ATOA WITO KWA VIJANA NA WANANCHI NJOMBE KULINDA AMANI



Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka,akizungumza katika Ibada ya Jumamosi katika Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Njombe Mjini.


Na Mwandishi Wetu, Njombe


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka vijana wa kizazi kipya (Gen-Z) na wananchi kwa ujumla kuimarisha mshikamano na kuilinda amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika Ibada ya Jumamosi katika Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Njombe Mjini, RC Mtaka amesema vijana wana nafasi kubwa katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa kisiwa cha amani.

“Vijana wetu wa Gen-Z wana wajibu wa kulinda amani ya Tanzania; ninyi ndiyo kizazi kinachobeba matumaini na sura ya taifa letu,"amesema.

Aidha, ameongeza kuwa amani ni matokeo ya haki na uwajibikaji wa kila mwananchi.

“Amani ni tunda la haki na wajibu, ni msingi thabiti wa maendeleo yetu kama jamii na kama taifa. Tuna wajibu wa kuilinda amani ya nchi yetu kwa wivu mkubwa… ni jukumu letu vijana wa leo kuitunza amani yetu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo,"amesema.

Akizungumzia hali ya usalama mkoani Njombe, Mtaka amewahakikishia wananchi kuwa mazingira bado ni salama na hakuna viashiria vya kuvuruga utulivu.

“Mkoa wetu bado upo salama, hauna matishio ya kihalifu. Tunaendelea kujenga mazingira thabiti ya ulinzi wa watu na mali ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji. Usalama huu utaongeza imani kwa wawekezaji kuendelea kuchagua Njombe kama sehemu sahihi ya kuweka mitaji,” amesema.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za mapema pale wanapohisi au kuona dalili za kuvunjika kwa amani.

“Wananchi wenzangu, mkiona au kuhisi dalili yoyote hata ndogo inayoashiria uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa eneo lenu au maisha ya mtu, basi mtoe taarifa mapema. Ulinzi shirikishi huanza na wanajamii mmoja mmoja,” amesisitiza.

Amehimiza umoja, uzalendo na uadilifu wa wananchi wote ili kuendelea kujenga Njombe yenye fursa, utulivu na maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment